RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amezisihi Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) kuongeza ushirikiano kwenye ufanisi wa kazi zao.
Dk. Mwinyi ametoa nasaha hizo, Ikulu,
Zanzibar alipozungumza na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Francis
Chalamila aliefika kujitambulisha kufuatia uteuzi wa kutumikia nafasi aliyonayo
uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan
hivi karibuni.
Rais Dk. Mwinyi amezishauri taasisi hizo
mbili kuzidisha ushirikiano hasa kwenye miradi ya kimkakati ya Mendeleo kwa
maslahi ya taifa.
Aidha, Dk. Mwinyi amempongeza Mkurugenzi
Chalamila kwa uteuzi alioupata na kumtakia heri kwenye majukumu yake mapya.
Pia Rais Dk. Mwinyi amesifu jitihada za
ZAECA kwa kuendeleza ufanisi wa makujukumu yao hasa kwenye miradi ya Serikali kwa
wanawajibika ipasavyo.
Akizungumza kwa wakati huo bw. Chalamila
alimuahidi Rais Dk. Mwinyi kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya ZAECA na
TAKUKURU katika kufanikisha majukumu yanayowalazimu.
Amesema, TAKUKURU na ZAECA wanashirikiana
kwenye mambo mengi tokea waliposaini mkataba wa ushirikiano wao mwaka 2012, ikiwemo
kujengeana uwezo, kusihirikana kwenye masuala ya uchunguzi wa kazi zao,
kushiriki mikutano ya pamoja ya kikanda na kitaifa.
Vile vile bw. Chalamila alisifu na
kupongeza juhudi za maendeleo makubwa zilizofikiwa na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dk. Mwinyi.
Alisema, mbali na majukumu mengine
walivyonayo TAKUKURU na ZAECA imekua rahisi kwao kushirikiana hasa kuwadhibiti
wahalifu wa pande mbili za Muungano wanaojaribu kukimbilia kwenye mipaka ya
sehemu hizo Bara na Visiwani.
Bw. Chalamila pia alimuahidi Rais Dk.
Mwinyi na Rais Dk. Samia kuendeleza maono yao, na ushauri wao katika mapambano
dhidi ya vitendo vya rushwa na uhujumu uchumi kwa kushirikiana na ZAECA.
Sambamba na kuendeleza mikakati na
uchunguzi kwenye miradi ya maendelo na kumuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kwamba
wataendelea kusimamia miradi hiyo na kuhakikisha inakamilika kwa viwango vinavyostahiki
na kuhakikisha thamani ya fedha za miradi hiyo inaonekana.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Dk. Samia Suluhu Hassan alimteua bw. Chalamila kushika wadhifa alionao sasa
Ogasti 14 mwaka huu na kumuapisha Ogasti 15 mwaka huu.
IDARA YA MAWASILINO, IKULU ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment