Habari za Punde

serikali kupitia ofisi ya Makamu wa pili wa Rais itaendelea kutoa ushirikiano wa hali ya juu kwa Wizara ya Muungano na Mazingira na Wizara nyengine za Muungano

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema kuwa serikali kupitia ofisi ya Makamu wa pili wa Rais itaendelea kutoa ushirikiano wa hali ya juu kwa Wizara ya Muungano na Mazingira  na Wizara nyengine za Muungano ili kuleta ufanisi nzuri wa kazi kwa pande zote mbili za Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira wakiongozwa na Waziri wa Wizara hio Dkt. ASHATU K. KIJAJI waliofika Ofisini kwake Vuga kwa lengo la kujitambulisha baada ya  kuteuliwa mwezi July mwaka huu.

Mhe.Hemed amesema  Wizara vya Muungano na Mazingira ndio Wizara ambayo Watanzania wote wanaitegemea kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya ya kuwaunganisha Watanzania wa pande zote mbili za Muungano hivyo wataendelea kutoa ushirikiano wa hali ya juu ili kuudumisha Muungano huo ambao umeasisiwa na waasisi wa Taifa hili Mwalimu J.K Nyerere na hayati Sheh Abeid Amani Karume.

Makamu wa Pili wa Rais amesema Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania na ya Awamu ya Nane ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari wamezitatua kero nyingi za Muungano  hivyo ni wajibu wa kila Mtanzani kuulinda na kuuenzi Muungano ulipo wa Tanganyika na Zanzibar.

Mhe. Hemed amesema kuwa kuimarika kwa Muungano  kunasababishwa na makubaliano ya viongozi wa pande zote mbili hivyo ameuwelekeza Uongozi wa Wizara hio kuhakikisha wanafanya kazi kwa ushirikiano kwa pande zote mbili za muungano kwa lengo la kuudumisha muungano huo kwa maslahi mapana ya watanzania.

Sambamba  na hayo Makamu wa pili wa Rais Zanzibar amesema kuwa kwa sasa viongozi wa Wiraza zote za Serikali ya Jamuhuri ya Muungano na Wiongozi wa Wizara za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wanashirikiana kwa hali ya juu katika kuwatumikia wananchi wa pande zote mbili na kuwaletea maendeleo hivyo atahakikisha kuwa Muungano huu utaendelea utaendelea kudumu milele kwa faida ya vizazi vya sasa na baadae.

Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. ASHATU .K. KIJAJI amesema kuwa wizara imejipanga katika kuwatumikia Watanzania wa pande zote mbili za Muungano ili kuweza kufikia malengo ya Viongozi wakuu wan chi ya kuwaletea maendeleo wananchi wote.

Waziri Dkt.  KIJAJI amesema katika kutunza mazingira Wizara imejipanga kutoa Elimu kwa wananchi wa pande zote mbili za Muungano juu ya matumizi mazuri ya Nishati safi ya kupikia ili kutunza mazingira kwa maslahi mapana ya wananchi pamoja na kupambana na mabadiliko ya Tabia nchi kwenye mazingira yaliyozunguka makaazi ya watu.

Dkt. Kijaji amesema kuwa wizara ya  Muungano na Mazingira kwa kushirikiana na Wizara inayohusiana na Masuala ya muungano ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari wameshaweka mkakati maalumu wa kukutana kila mwezi kwa lengo la kujadili masuala mbali mbali ya Muungano kwa maslahi mapana ya wananchi wa pande zote mbili za muungano.

 

Imetelowa na kitengo cha Habari ( OMPR)

Leo tarehe….26.09.2024

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.