Dk. Mwinyi ameyasema hayo, alipozungumza katika kongamano maalumu
la Umoja wa Wazazi Tanzania la kupongeza juhudi za miaka minne ya uongozi wake
na Serikali anayoiongoza ya awamu ya nane kwa maendeleo na mafanikio makubwa
yaliyopatikana hapa nchini.
Aidha, Dk. Mwinyi ameutaka Umoja huo kuhakikisha WanaCCM watakaojitokeza
kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapigakura, wanatumia haki yao ya
kikatiba ya kupiga kura siku ya uchaguzi, 2025.
Alifahamisha, kwa kufanya hivyo CCM, itakuwa na uhakika wa
kupata wingi wa kura na ushindi mkubwa usio na mashaka na kuondosha malalamiko
ya wapinzani kila wanaposhindwa uchaguzi.
Rais Dk. Mwinyi amesema, CCM ina kila sababu ya kushinda
uchaguzi ujao wa 2025 kutokana na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama
hicho 2020 -2025 iliyovuka malengo katika sekta mbalimbali za maendeleo.
Makamu Mweyekiti huyo wa CCM Zanzibar, amewasisitiza wanachama
na viongozi wa jumuiya zote za Chama hicho kuendelea kujipanga vema na
kufanyakazi za chama kwaajili ya uchaguzi mkuu ujao.
Alisema, CCM inaridhika na kazi inayofanywa na jumuiya ya wazazi
na kutaka kuendelezwa ili kuwaunganisha wanachama kuwa na mwelekeo mmoja kwa
dhamira ya kuendelea kuongoza nchi kwa miaka mingi ijayo.
Pia, amepongeza uamuzi wa Jumuiya ya Wazazi kuandaa Kongamano
maalum la kumpongeza kwa mafanikio ya miaka minne ya uongozi wake, na kuongeza
kuwa hatua hiyo imemuongezea ari na motisha yeye na watendaji Serikalini ya
kufanya mambo makubwa zaidi kuwaletea wananchi maendeleo.
Akizungumza kwenye Kongamano hilo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Wazazi Taifa, Fadhil Rajab Maganya, ameeleza kuwa Jumuiya itaendelea kuwa
mstari wa mbele kuhakikisha wagombea wote wa CCM wanashinda kwenye uchaguzi
mkuu ujao pia ameelezea dhamira ya Jumuiya hiyo ya kujenga jengo la kisasa la
ghorofa nne kwaajili ya ofisi za jumuiya hiyo katika eneo la sasa la ofisi ya Jumuiya
hiyo.
Aidha, Jumuiya hiyo imekiomba Chama Cha Mapinduzi kuwaongezea
idadi ya wajumbe wa viti maalumu kwenye mabaraza yao ya maamuzi.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu CCM Taifa, Balozi. Emmanuel
Nchimbi, Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar, Muhamed Said Muhamed Dimwa, amesema CCM
inaridhishwa na kiwango cha juu cha utekelezaji wa Ilani ya Chama hicho unaofanywa
na Serikali na kumuhakikisha Dk. Mwinyi kwamba, inaamini kuwa Dk. Hussein
Mwinyi ndie atakaekuwa mgombea pekee wa chama hicho kwa nafasi ya Rais wa
Zanzibar, 2025 hadi 2030.
Amesifu uongozi wa Dk. Mwinyi kwa kuendeleza jitihada za
kuwaunganisha watu, maendeleo ya uchumi yanayonufaisha wananchi wote, kuzalisha
ajira rasmi na siozo rasmi, kuajiri wataalamu wa fani zote, kuimarisha sekta ya
huduma ikiwemo Afya, elimu na miundombinu ya maji na barabara za kisasa, viwanja
vya ndenge Unguja na Pemba, Sekta ya Uchumi wa Buluu na kuendeleza mapambano
dhidi ya rushwa.
Naye, Mjumbe wa Halimashauri Kuu ya CCM, Taifa na Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema kazi inayofanywa na Dk.
Mwinyi katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake imewaondoshea Wazanzibari
matatizo kwa kiwango kikubwa katika nyanja mbalimbali za kijamii nakueleza kuwa
kwa kuzingatia mafanikio hayo, Chama kinakusudia kuandaa mpango maalumu wa
kuyaonesha mafanikio hayo kwa wananchi kuanzia ngazi ya wadi, Shehia, tawi hadi
jimbo.
Kongamano hilo, lililokuwa na kauli mbiu "Mzazi
mshike mwanao muhimize 2025 akapige Kura" liliandaliwa na Jumuiya
ya Wazazi Tanzania ambayo imekua ya kwanza kufungua wiki ya kupongeza mafaniko
ya miaka minne ya Serikali ya awamu ya nane ya uongozi wa Dk. Mwinyi.
Jumiya hiyo pia ilimkabidhi Makamu Mwenyekiti wa CCM, Zanzibar
Dk. Hussein Mwinyi shilingi milioni 2.1 kwaajili ya kuchukulia fomu ya kugombea
Urais wa Zanzibar wakati utakapofika na kupendekeza kwa Chama hicho kutoa fomu
moja tu ya ugombea wa urais wa Zanzibar mwaka 2025.
Kwenye Kongamano hilo kuliwasilishwa mada mbalimbali zilizoeleza
mchango wa Chama Cha Mapinduzi katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama
hicho, 2020-2025 ndani ya miaka minne ya uongozi wa Dk. Mwinyi, Mchango wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kufanikisha utekelezaji wa Ilani hiyo,
aidha, Mafanikio yaliyopatikana kwenye sekta zote za maendeleo ikiweo Elimu,
Afya, Miundombinu ya maji, barabara, viwanja vya ndege, mawasiliano na Ustawi
wa Wazee.
IDARA
YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment