Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla amesema Taaluma ua Ukaguzi wa ndani ni msingi wa uadilifu na mafanikio kwa Taasisi za Umma na binafsi zinashuhulika na Taaluma hio.
Ameyasema hayo kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika ufunguzi wa Mkutano wa Kumi na Saba (17) wa Wakaguzi wa ndani uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano ya Kimataifa jijini Arusha.
Amesema kutokana na jukumu la ukaguzi wa ndani kuwa ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa ni wajibu wa wakaguzi wa ndani kukusanya nguvu za pamoja katika kujenga mustakbali wenye mafanikio zaidi, usawa endelevu na utawala bora nchini.
Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar amesema kuwa wakaguzi wa ndani ni mabingwa wa utawala bora, walinzi wa uwadilifu, na ni watu wenye viwango vikubwa vya maadili hivyo huhakikisha kuwa taasisi zao zinafanya kazi kwa viwango vikubwa, uwajibikaji, uwazi na uaminifu kwa wananchi, wafanyabiashara na washirika wa Kimataifa ili kuisaidia nchi kupiga hatua kimaendeleo.
Mhe. Hemed amesema Serikali inatambua umuhimu mkubwa wa kudumisha uhuru na usawa wa wakaguzi wa ndani hivyo Serikali iko imara katika kuzingatia kanuni za ukaguzi wa ndani ili kuhakikisha wanafanya kazi zao bila ya ushawishi usiofaa na kutokuingiliwa katika majukumu yao ya kila siku.
Aidha, Makamu wa Pili wa Rais amewahakikishia wakaguzi wa ndani kuwa Serikali inatambua na kuunga mkono kikamilifu jukumu muhimu la ukaguzi wa ndani hivyo itahakikisha inaimarisha mfumo unaowezesha kazi zao, kuongeza uwezo wa ukaguzi wa kitaaluma na kukuza utamaduni wa uwajibikaji katika Taasisi zote.
Sambamba na hayo Mhe.Hemed ametoa wito kwa wakaguzi wa ndani kuutumia Mkutano huo katika kujadiliana na kubadilishana mawazo chanya yatakayoleta uvumbuzi na maarifa zaidi katika kuendeleza Taaluma hio kwa mustakabali mwema wa maendeleo ya Taasisi zetu na Taifa kwa ujumla.
Nae Rais wa Taasisi ya Ukaguzi wa Ndani Tanzania ( I I A )Dkt. ZALIA NJEZA amesema lengo la kuwepo kwa Mkutano wa wakaguzi wa ndani ni kujadiliana njia mbali mbali zitakazo wawezesha kufanya kazi zao kwa uadilifu na uwajibikaji na kuisaidia Serikali kufanya kazi za ukaguzi kwa ufanisi na kwa viwango vya hali ya juu.
Dkt ZALIA amesema Taasisi ya Ukaguzi wa Ndani Tanzania imekuwa na jukumu la kuhakikisha wanachama wake wanaendelezwa kielimu, kutanua wigo wa mtandao wa wanataaluma ya ukaguzi ndani na nje ya nchi pamoja na kuwajengea uwezo wa kufanya kazi zao kwa kufuata maadili na uamifu ili kuisaidia Serikali katika uwajibikaji hasa wa udhibiti wa matumizi ya rasilimali fedha.
Amesema Taasisi ya Wakaguzi wa ndani itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Serikali zote mbili pamoja na wadau wao ili kurahisisha ufanyaji kazi kupitia taaluma hio kwa kuwa na Wakaguzi wa ndani wenye taaluma, ujuzi na viwango vye ubora katika ukaguzi wa ndani.
Kwa upande wake Mkaguzi Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania CPA BENJAMIN MASHAURI MAGAI amesema Ukaguzi wa ndani ni eneo muhimu endapo litaimarishwa na litaisaidia Serikali na Taasisi binafsi kuangalia rasilimali za nchi, udhibiti wa mifumo ya ndani , viashiria vya upotevu wa rasilimali na kusimamia ulinzi katika matumizi ya rasilimali kwa Taasisi zote nchini.
CPA .MASHAURI amesema wakaguzi wa ndani nchini wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo uhaba wa vifaa na rasilimali fedha hada pale wanapolazimika kufanya kazi nje ya maeneo yao ya kazi jambo ambali linawapa wakati mgumu katika kutimiza majukumu yao kwa uweledi na ufanisi zaidi hivyo wameziomba serikali kuweza kuwatatulia changamoto zinazowakabili ili kuwarahisishia ufanyaji wa kazi zao.
Akitoa salamu za Mkoa wa Arusha kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo CRISTIAN PAUL MAKONDA, Mkuu wa Wilaya ya Munduli FESTO SHEM KITEANGWA amesema Serikali imathamini jukumu muhimu linalifanywa na wakaguzi wa ndani katika kuisaidi Serikali kupiga hatua za kimaendeleo hasa katika udhibiti wa rasilimali katika Taasisi za umma na Taasisi binafsi nchini.
KISANGA amesema Mkutano huo ukawe chachu na kutoa fursa ya kusaidiana na kuendelezana kitaaluma, kubadilishana uzoefu pamoja na kuweka mikakati imara ya kufikia malengo ya Taasisi hiyo na Taifa kwa ujumla.
Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amekagua mabanda ya maonesho na kujionea kazi mbali mbali zinazofanywa na wakaguzi wa ndani walioshiriki katika ufunguzi wa Mkutano wa Kumi na Saba(17) wa Taasisi ya Wakaguzi wa ndani Tanzania kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi yaliyopo nje ya Ukumbi wa Mikutano ya Kimataifa jijini Arusha.
Imetolewa na Kitengo cha Habari ( OMPR)
Leo tarehe 03 / 10 / 2024.
No comments:
Post a Comment