Makamu wa
Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, amesema kwamba Zanzibar
inatatizo kubwa la uharibifu wa mazingira linalohitaji jitihada za pamoja kati
ya wadau, wahisani na washirika mbali mbali ili kuweza kulikabili ipasavyo na
kupunguza athari zitokanazo na changamoto hiyo.
Mhe. Othman
ameyasema hayo huko nyumbani kwake Chukwani Zanzibar alipofanya mazungunzo na
Ujumbe kutoka Bodi ya Wakurugenzi ya
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), ulioongozwa na
Mwenyekiti wake Profesa Esnati Osinde Chaggu.
Mhe. Othman
amesema kwamba changamoto hiyo inayotokana na athari za mabadiliko ya tabia
nchi ni vita kubwa ya kimazingira na ni jambo ambalo haliwezi kushughulikiwa
ipasavyo pasipo jitihada za pamoja kati ya wadau, wahisani pamoja na wataalamu
sambamba na kupatikana rasilimali za aina mbali mbali.
Amefahamisha
kwamba maeneo mengi yameharibika na
kwamba ni vigumu kwa Zanzibar pekee kwa
nguvu za waliopewa dhamana ya usimamizi wa mazingira kuweza kuyarejeshea
hali yake ya uasili pasipo na jitihada za pamoja kutoka ndani na nje ya nchi.
Mhe. Othman
ameutaka uongozi wa Bodi hiyo kuhakikisha wanalichukua suala la changamoto ya
uharibifu wa mazingira kwamba ni la wote hasa kwavile katika mtazamo wa
kimataifa Tanzania ndio mlango wa wakutambuliwa.
Amesema
kwamba hivi sasa zaidi ya maeneo 145 hapa Zanzibar yamehakabiliwa na changamoto
kubwa ya kuharibika kimazingira ambapo jitihada za pamoja ndio njia nyepesi ya
kusaidia kukabiliana na hali hiyo.
Akizungunzia
tisho la uhaba wa maji kunakotokana na athari hizo, Mhe. Othman amesema kwamba
Zanzibar kwa asilimia 100 inategemea vyanzo vya maji kutoka aridhini na kwamba
hali hiyo kama haikuchukuliwa tahathari mapema upo uwezekano wa changamoto hiyo
kuongezeka.
Amesema
kwamba hali hiyo inaweza kuathiri pia sekta ya utalii ikizingatiwa kwamba
Zanzibar hivi sasa inahoteli zaidi ya 600 za daraja tofauti ambapo mahitaji ya
sekta hiyo , pasipo na hifadhi bora ya mazingira nayo inaweza kuathirika na pia
idadi ya wageni wanaotembelea nchi inaweza kupungua iwapo mazingira
hayaridhishi.
Ameishauri
Bodi hiyo kwamba suala la mazingira ni fursa muhimu ya kuwezesha kufanya kazi pamoja
kwa taasisi zilizopewa jukumu la usimamizi wa mazingira kati ya bara na
Zanzibar ili juhudi hizo ziweze kufanikiwa.
Akizngunzia
suala la ardhi , amesema kwamba sehemu kubwa ya ardhi inayohitajika kwa kilimo
imepo Magharib mwa visiwa vya Unguja na pemba na kwamba tayari imeshatumika kwa
shughuli za makazi ya binaadamu na kwamba ni masuala yanayoongeza changamoto ya
athari za kimazingira Zanzibar.
Naye
Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Profesa Isnati Osinde Chaggu , amesema kwamba chombo
hiyo kimepewa jukumu na Mamlaka ya kutafiti , kufuatilia pamoja na mambo
mengine kuhakikisha kwamba masuala yote
ya mazingira nchini Tanzania yanasimamiwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu
zilizowekwa.
Amesema
kwamba mabadiliko ya taibia nchi yanahitaji kila juhudi katika kuhakikisha
kwamba athari zinazotokana na tatizo hilo haziongezeki hasa kwa vile masuala ya
tabia nchi hayana mipaka zaidi ya kukabiliwa kwa juhudi za pamoja.
Kwa upande
wake Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo Immaculate
Sware Semesi, amesema kwamba suala la uchumi wa bluu, mafuta na gesi asilia linalohusisha
masuala ya sera ya uchumi wa matumizi ya rasilimali ya bahari kwa wananchi na
taifa kwa jumla halina mipaka kutoka pande zote za muungano na kwamba linahitaji kusimamiwa kwa
juhudi za pande zote mbili.
Naye
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar Sheha Mjaja Juma,
amesema kwamba ofisi yake inaendelea kujenga mashirikiano na wenzao wa Tanzania
Bara katika kuhakikisha kwamba suala la mazingira linasimamiwa ipasavyo nan chi
inaendelea kuwa salama.
Imetolewa
na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kupitia ofisi ya Makamu wa
Kwanza wa Rais wa Zanzibar leo Jumamosi tarehe 12. Oktoba 2024.
No comments:
Post a Comment