Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (๐ฆ๐๐๐) inaendesha mafunzo kwa Ujumbe wa Uangalizi wa Uchaguzi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC Electoral Observation Mission - SEOM) katika uchaguzi Mkuu wa Botswana unaotarajiwa kufanyika tarehe 30 Oktoba, 2024.
Mafunzo hayo maalum kwa Ujumbe wa SEOM yanafanyika
jijini Gaborone, Botswana kuanzia tarehe 17 hadi 20 Oktoba 2024 ikiwa ni sehemu
ya maandalizi ya uangalizi wa Uchaguzi Mkuu katika Jamhuri ya Botswana.
Tanzania ambaye ni Mwenyekiti wa Asasi
ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC inaongoza ujumbe wa waangalizi hao ambapo Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tazania na Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na
Usalama ya SADC, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amemteua Waziri Mkuu
Mstaafu wa Tanzania Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda kuongoza Misheni hiyo ya uangalizi
katika Uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Botswana.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo
hayo yaliyofanyika tarehe 17 Oktoba, 2024 kwa niaba ya Ofisi ya Mratibu wa
Masuala ya SADC Tanzania Bi. Lilian Mukasa amezishukuru Nchi Wanachama kwa
kutuma wajumbe wao kwa ajili ya kuunda timu ya uangalizi ya SADC na kubainisha
kuwa mafunzo hayo yataendeshwa na wakufunzi kutoka Sekretarieti ya SADC na
Taasisi ya Uchaguzi kwa Demokrasia Endelevu Afrika (EISA). Ameeleza kuwa
mafunzo hayo yatajikita katika masuala ya mbalimbali ya kisera na kisheria ya
Botswana, kikanda na kimataifa yanayotumika katika kusimamia uchaguzi ikiwa ni sehemu
ya juhudi za kuimarisha demokrasia na utawala bora katika kanda.
Amesema mafunzo hayo yatawapatia waangalizi
maarifa na kuwawezesha kufahamu viwango
na kanuni za uchaguzi wa kidemokrasia; Kanuni na Miongozo ya SADC inayoongoza
Uchaguzi wa Kidemokrasia iliyorekebishwa; uangalizi wa uchaguzi katika hali za
dharura za afya ya umma (mfano janga la COVID-19); kukuza uelewa kuhusu
mzunguko wa uchaguzi; tathmini ya hatua za mzunguko wa uchaguzi; mifumo ya
uchaguzi katika kanda ya SADC; ujuzi wa ukusanyaji taarifa; na matumizi ya
kompyuta kibao, pamoja na ukusanyaji na utumaji wa taarifa (data).
Katika Uchaguzi mkuu huo wananchi wa
Botswana watawachagua Wabunge wa Bunge la 13 la nchi hiyo na wajumbe wa Mabaraza
ya Mitaa ambapo viti 61 vya Bunge la Taifa na viti 609 vya mabaraza ya mitaa vitashindaniwa.
SEOM inatarajiwa kupeleka waangalizi wa uchaguzi katika wilaya, miji na majiji
yote nchini Botswana.
No comments:
Post a Comment