Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapindizi Dk.
Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuongeza bajeti ya Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Amali kwani ni sekta ya kipaumbele kwa maendeleo ya nchi.
Dk. Mwinyi ameyasema hayo alipofungua Skuli mpya ya Sekondari ya
ghorofa tatu, Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini Unguja, ikiwa ni mwendelezo wa wiki
ya kupongeza juhudi za Serikali ya awamu ya nane kufuatia mafanikio makubwa
yaliyopatikana chini ya uongozi wa miaka minne ya Dk. Mwinyi.
Amefahamisha kuwa uzinduzi wa skuli hiyo ni kuimarisha mifumo na
miundombinu ya elimu ili kufanikisha mageuzi makubwa yanayoendana na teknolojia
ya sasa ulimwenguni.
“Hii ni dunia ya teknolojia, hivyo tunaweka kipaumbele katika
kuimarisha teknolojia ili vijana waende sambamba na mabadiliko ya dunia na
kuongeza ufaulu wao” ameeleza Rais Dk. Mwinyi.
Amesema fungu kubwa la bajeti hiyo litaelekezwa zaidi kwenye
kuimarisha mifumo ya elimu, ujenzi wa miundombinu ya skuli za kisasa ikiwemo
maabara, vyumba vya kompyuta, maktaba, kumbi za mikutano ambazo hutumika kwa
kufanyia mitihani ya wanafunzi.
Dk. Mwinyi amesisitiza kuwa hadi sasa Wizara ya Elimu imetengewa
bajeti ya shilingi bilioni 830 ambayo inatarajiwa kuongezeka hadi kufikia
shilingi Trilioni moja kutoka bajeti ya miaka mitatu nyuma ya bilioni 83.
Aidha, amebainisha, tayari Serikali imejenga madarasa 2738 kwa
kuvuka lengo la Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020 - 2025 ambayo ilielekeza
kujengwa madarasa 1500, hatua hiyo inakusudia kutekeleza adhma ya Serikali ya
kuona wanafunzi wanasoma kwa mkondo mmoja chini ya wanafunzi 45 katika darasa
moja huku serikali ikiweka mkazo zaidi kwenye masomo ya hisabati na sayansi.
“Kuanzia sasa lazima darasa lisizidi watoto 45 nchi nzima”
alisisitiza Dk. Mwinyi.
Kuhusu maslahi ya walimu Rais Dk. Mwinyi amesema, Serikali
itaendelea kuongezaa hasa kwa wanafanyakazi wenye mazingira magumu, huku
akiwasisistiza vijana kusoma zaidi kwani Serikali yao inaendelea kuwajengea
mazingira mazuri.
Akizungumzia ajira mpya za walimu, Dk. Mwinyi ameeleza tayari
Serikali imeajiri walimu 3600 na inalenga kuongeza ajira za walimu zaidi hasa
kwa kada za sayansi na hesabati.
Hata hivyo, ameeleza kufarajika kwake na mafanikio makubwa
katika sekta ya Elimu ambayo yamechangia kuongeza kiwango cha ufaulu kwa
wanafunzi kufikia asilimia 96.6 kwa kidato cha sita na asilimia 88 kwa kidato
cha nne kutoka asilimia 55 kabla ya miaka minne ya uongozi wake.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla
amesema, ujenzi wa Skuli za ghorofa, Kaskazini, Unguja umewaletea Faraja wazazi
na wanafunzi wa mkoa huo kwa tatizo la umbali wa kufuata elimu katika skuli za
mjini.
Amenasihi kuwa njia sahihi ya kuleta uchumi imara na maendeleo
kwa Taifa ni kuwekeza kwenye elimu kwa wote kwani maedeleo hayana Chama, kwa
mustakbali mwema wa kuyatunza na kulinda. Hivyo, amewasisitiza wazazi na walezi
kufanya kazi za ziada kusimamia elimu ya watoto wao kwani suala la kuipatia
elimu jamii sio la chama ni la wote, sambamba na kuionya jamii kuepuka
upotoshwaji unaofwanywa na watu wasioitakia nchi maendeleo ambao wamekua
wakisambaza taarifa potofu.
Naye, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Muhamed
Mussa, amemsifu na kumpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kubeba jukumu la kuiletea
mageuzi makubwa Sekta ya Elimu, kwa kuweka Fedha nyinyi za kutekelezwa miradi
mbalimbali ya elimu.
Amesema, jitihada hizo ikiwemo kuwekeza vifaaa na miundombunu ya
kisasa ya kufundishia zitasaidia kwenye mchango wa maendeleo ya taifa kwa kutoa
wataalamu wakutosha watakaokuwa tayari kushindana katika soko la ajira
ulimwenguni.
Akitoa taarifa ya kitaamu ya ujenzi wa Skuli mpya ya Sekondari
ya Mkokotoni ya ghorofa tatu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali,
Khamis Abdalla Said amesema, ulianza mwezi Mei 2023 na kukamilika Oktoba 2024
umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 6.1, una madarasa 42, vyoo 52, chumba cha
kompyuta, maabara, maktaba. Skuli hiyo itachukua wanafunzi 1890 kwa mkondo
mmoja.
Mkuu wa Mkoa Kaskazini, Unguja, Rashid Hadid Rashid amesema
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetenga shilingi bilioni 50.2 kwaajili ya
miradi ya Elimu tu kwa Mkoa huo ambapo hadi sasa zaidi ya shilingi bilioni 40.9
zimetumika kwa ujenzi wa skuli sita za ghorofa kwa maeneo mbalimbali ya Mkoa
huo ikiwemo Skuli ya ghorofa ya Bumbwini Misufini iliyogharimu bilioni 6.1, Skuli
ya Donge shilingi bilioni 4.6, Tumbatu bilioni 7.025 na ujenzi wa Skuli ya
Ghorofa Gamba unaoendelea utagharimu bilioni 11.
IDARA
YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment