Habari za Punde

Taasisi za Serikali na binafsi zaombwa kuipiga jeki Jumuiya ya Wajane Zanzibar (ZAWIO)

 Na Takdir Ali. Maelezo. 04.10.2024.

 

Taasisi za Serikali na binafsi nchini zimeombwa kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Jumuiya ya Wajane Zanzibar (ZAWIO) katika kuwawezesha na kuwaenua Wajane kiuchumi.

 

Wito huo umetolewa na Jaji wa Mahakama kuu Zanzibar Mhe. Fatma Hamid Mahmoud wakati alipokuwa akifunguwa mafunzo ya Wajane wanaofanya Biashara katika Soko la Jumbi na Mombasa ili kuweza kuendesha biashara zao kwa ufanisi.

 

Amesema Mashirika na Taasisi nyingi zinatoa kipaombele zaidi kwa Vijana, Wanawake na Watu wenye ulemavu na kulisahau kundi la Wajane ambalo linahitaji kusaidiwa kwa kiasi kikubwa.

 

Aidha amesema pamoja na kuwa Wajane wanaweza kuingizwa katika kundi la Wanawake lakini baadhi yao wanajitegemea wenyewe na wengi wao hawana kazi za uhakika za kuwapatia kipato cha kuendeleza Maisha yao kila siku.

 

Hata hivyo amesema kutokana na Changamoto mbalimbali wanazozipata kuna uwezekano mkubwa wa kundi hilo kujiingiza katika mambo yasiofaa ili kukidhi mahitaji yao.

 

‘‘Tunajuwa kuna kundi la Wajane ambao wanapata matatizo ya akili kutokana na msongo wa Mawazo kwa kushindwa kukabiliana na shida za Maisha na lakini hata pia wengine kujiingiza katika masuala ya mapenzi”alisema Jaji Fatma.

 

Hata hivyo ameipongeza taasisi ya Wajane kwa kuanzisha program maalum za kuwasaidia kufanya shughuli za Uchumi kwa kuwaunganisha na Mabenk ili kuweza kuwapatia Mitaji.

 

Mapema akitoa maelezo Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wanawake Zanzibar (ZAWIO) Tabia Makeme Mohammed amesema mafunzo hayo, yamejikita zaidi kuwapatia elimu ya mbinu za kuanzisha na kuendeleza Biashara,kujuwa fursa mbalimbali zilizopo kupitia Jumuiya hiyo na kujikinga na VVU na magonjwa ya Afya ya akili.

 

Aidha amesema mafunzo hayo pia yatawasaidia kujuwa haki zao za msingi ikiwemo taaluma juu ya Afya ya akili, Utawala wa Sheria, usawa wa vyombo vya Dola na kugombania nafasi mbalimbali za Uongozi ili kusukuma gurudumu la Maendeleo.

 

Nao washiriki wa mafunzo hayo wameipongeza ZAWIO kwa kuandaa mafunzo hayo kwani yamepata elimu ya masuala mbalimbali kama vile Ukimwi, Afya ya akili sambamba na kuomba kutolewa mara kwa mara ili yazidi kuwasaidia.

 

Hata hivyo amewaomba Wajane wenzao wasijiweke nyuma, wajitambuwe, wafanye kazi kwa bidii na wasikubali kurubuniwa na Watu wasiopenda maendeleo yao.

 

Mafunzo hayo ya siku moja ya kuwajengea uwezo Wajane wanaofanya Biashara katika Soko la Jumbi na Mombasa, yameandaliwa na Jumuiya ya Wajane Zanzibar (ZAWIO) na kudhaminiwa na Taasisi ya WCF.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.