Habari za Punde

SERIKALI YAONGEZA BAJETI YA ELIMU 522.6%

 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akikata utepe kuifungua Skili ya Sekondari ya Konde ya ghorofa tatu (kushoto kwa Rais ) Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla na (kulia kwa Rais) Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe.Lela Mohammed Mussa na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe.Zuberi Ali Maulid, ikiwa ni Shamra Shamra za Kuadhimisha Miaka Minne (4) ya Serikali ya Awamu ya Nane (8) Madarakani iliyofunguliwa rasmi leo 1-11-2024.

SERIKALI ya Mapindizi ya Zanzibar imesema imeongeza bajeti ya Maendeleo kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kutoka TZS bilioni 83.2 mwaka 2021/22 hadi kufikia TZS bilioni 518 mwaka 2024/2025.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapindizi Dk. Hussein Ali Mwinyi ametangaza bajeti hiyo alipofungua Skuli mpya ya Ghorofa tatu, Skuli ya Sekondari ya Konde, Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini, Pemba ikiwa ni mwendelezo wa kupongeza miaka minne ya mafanikio ya Serikali ya Awamu ya nane anayoiongoza.

Alisema, bajeti hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 522.6. ambayo imesaidia kufanikisha utekelezaji wa miradi mingi ya kimkakati inayolenga kuimarisha elimu na kuweka misingi imara ya maendeleo ya muda mrefu ya Taifa.

Akieleza bajeti ya Elimu ya Juu, Rais Dk. Mwinyi amesema Serikali imeongeza bajeti ya mikopo ya elimu ya juu kutoka TZS bilioni 11.5 kwa mwaka 2021/2022 hadi bilioni 33.4 mwaka 2024/2025 ambayo imeongeza idadi ya wanafunzi kutoka 4289 hadi kufikia 6,060.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi amesema hadi sasa Serikali tayari imejenga madarasa 2,773 sawa na zaidi ya asilimia 184 ya shabaha ya madarasa 1,500 yaliyoelekezwa kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, yenye uwezo wa kuchukua wastani wa wanafunzi 45 kwa shifti moja.

Ameeleza ujenzi huo pia umejumuisha ukamilishaji wa madarasa yaliyoanzishwa na wananchi, ujenzi wa madarasa mapya, pamoja na skuli 53 za chini na skuli 26 za ghorofa.

Pia, Rais Dk. Mwinyi ameeleza mafanikio hayo yanajumuisha ujenzi wa skuli 35 za ghorofa katika maeneo mbalimbali ambapo kwa Mkoa wa Kaskazini Pemba tayari ujenzi wa skuli za ghorofa sita umekamilika.

Akizungumzia hatua ya ujenzi wa madarasa mapya 2,037 Rais Dk. Mwinyi amesema, kazi ya ujenzi huo inaendelea na tayari Serikali imeajiri walimu 3531 pia Serikali imejenga maabara za Phisics, Chemistry na biology katika kuimarisha mitaala ya sayansi.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema ufunguzi wa Skuli mpya ya Sekondari Konde ni fursa adhimu kwa wananchi wa eneo hilo, hivyo aliwasihi wananchi wa Zanzibar kuendelea kumuunga mkono Rais Dk. Mwinyi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Khamis Abdalla Said amesema Skuli ya Sekondari Konde inauwezo wakuchukua wanafunzi 1890 wa wastani wa wanafunzi 45 kwa darasa moja kwa wakati mmoja, skuli hiyo imejumuisha madara 42, vyoo 52, maktaba, maabara, stoo, kumbi za mikutano, chumba cha kusalia na chumba cha TEHAMA.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Salama Mbarouk Khatib amepongeza juhudi za maendeleo zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya nane kwa kutimiza mambo ya msingi kwa wananchi.

Kwa upande wake Mwakilishi wa jimbo la Konde, Zawadi Amour ambae pia ni Naimu Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar, amesifu maendeleo makubwa yaliyofikiwa kwenye jimbo hilo kwa Shehiya zake za Makangale, Msuka na Kifundi ni jitihada za Serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Rais Dk. Mwinyi ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wake.

Amesema, jimbo la konde linajivunia maendeleo makubwa ya miundombinu ya barabara, ujenzi wa Skuli za msingi, pensheni kwa wazee 2277 wa jimbo hilo pamoja na ajira kwa vijana na kuweeshwa na serikali wananchi wa jimbo hilo iliwemo ajira za bodaboda.

IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.