Habari za Punde

TAFITI ZIFANYIKE KUWEZESHA MPANGO WA AFYA MOJA KUFANIKIWA - MAJALIWA.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitembelea mabanda ya maonesho wakati alipofungua  Mkutano wa Kitaifa wa Afya Moja kwenye ukumbi wa Nyasa katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha  (AICC), Novemba 4, 2024.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Sr Mary - John alipotembelea banda la maonesho la  SAPIEN  LABS - CERERAM iliyopo chini ya Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Arusha wakati alipofungua  Mkutano wa Kitaifa wa Afya Moja kwenye ukumbi wa Nyasa katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha  (AICC), Novemba 4, 2024.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama machapisho mbalimbali wakati alipotembelea banda la maonesho la Student One Health Innovation Club (SOHIC) wakati alipofungua  Mkutano wa Kitaifa wa Afya Moja kwenye ukumbi wa Nyasa katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha  (AICC), Novemba 4, 2024.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi na watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu baada ya kutembelea banda la maonesho la Idara ya Maafa wakati alipofungua  Mkutano wa Kitaifa wa Afya Moja kwenye ukumbi wa Nyasa katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha  (AICC), Novemba 4, 2024
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na viongozi mabalimbali wakiimba wimbo wa Taifa wakati alipofungua Mkutano wa Kitaifa wa Afya Moja kwenye ukumbi wa Nyasa katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha  (AICC), Novemba 4, 2024.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea kutoka kwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ummy Nderiananga tuzo ya shukurani kwa kuku bali kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Mkutano wa Kitaifa wa Afya Moja kwenye ukumbi wa Nyasa uliopo katika  Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha  (AICC), Novemba 4, 2024. Kushoto ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange na kulia ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza   wakati alipofungua  Mkutano wa Kitaifa wa Afya Moja kwenye ukumbi wa Nyasa katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha  (AICC), Novemba 4, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameziagiza idara na taasisi za utafiti na elimu ya juu ziendelee kufanya tafiti za kisayansi ili kutafuta suluhisho za changamoto zenye mwingiliano wa afya ya binadamu, afya ya wanyama, na afya ya mazingira. 

Ameongeza kuwa idara na taasisi za Serikali zinapaswa kutumia matokeo ya tafiti hizo katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya kitaifa.


Ametoa maagizo  hayo jana (Jumatatu, Novemba 04, 2024)  alipofungua Mkutano wa Kitaifa wa Afya Moja katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa  Arusha (AICC) Jijini Arusha.


Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa Taasisi zinazohusika na masuala ya afya ya jamii, wanyama na mazingira zitenge fedha na kuweka katika mipango ya taasisi hizo afua za kuthibiti magonjwa ya kizonotiki, usugu wa vimelea dhidi ya dawa, magonjwa yasiyoambukiza, mabadiliko ya tabia nchi, na usalama wa chakula.

 

“Wizara za kisekta, na Mamlaka za Serikali za Mitaa, andaeni mipango kazi na taratibu za usimamizi kwa ajili ya utekezaji wa mbinu ya Afya Moja kwa kuzingatia miongozo iliyopo ambayo imeweka bayana majukumu ya wadau wote”

 

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amezitaka taasisi hizo kufanya vikao vya mara kwa mara, tathmini ya utekelezaji wa pamoja wa afua mbalimbali ili zijulikane mapema na kupatiwa ufumbuzi.

 

"Idara na taasisi za utafiti na elimu ya juu ziendelee kufanya tafiti za kisayansi ili kutafuta suluhisho za changamoto zenye mwingiliano wa afya ya binadamu, afya ya wanyama, na afya ya mazingira."

 

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amesisitiza ushirikiano wa kisekta na jamii katika kupunguza na kudhibiti athari zitokanazo na majanga milipuko ya magonjwa, usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa, usalama wa chakula, magonjwa yasiyoambukiza, na matishio mengine ya afya ya jamii.

 

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga amesema, Ofisi ya Waziri Mkuu inaendelea kusimamia Dhana ya Afya Moja ili iendelee kupewa kipaumbele na wadau mbalimbali kwani suala hilo linagusa sekta nyingi.

 

Naye, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdala Ulega amesema Serikali kupitia wizara ya Kilimo imetenga shilingi bilioni 28, kwa lengo na dhamira ya kufanya kampeni ya chanjo kwa mifugo yote Nchini.

 

Awali, Naibu waziri wa Nchi OR- TAMISEMI Festo Ndugange, alisema utekelezaji wa mpango wa afya moja ni suala la muhimu katika kudumisha na kuimarisha afya ya jamii, hivyo wizara hiyo itaendelea kuahirikiana na wizara nyingine katika kukinga na kupambana na changamoto za magonjwa ambukizi kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.

 

 

(mwisho)

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,   

JUMANNE, NOVEMBA 5, 2024

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.