Kwa
niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja, Mkurugenzi
wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Kemilembe Mutasa leo Novemba 29, 2024 jijini
Dodoma akifungua Mkutano wa Kitaifa kuhusu mrejesho wa ushiriki wa Tanzania
katika Mkutano wa 29 wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP29), uliofanyika Novemba 11
hadi 22, 2024 Baku, Azerbaijan.
Tanzania imeahidiwa jumla ya Dola za Marekani milioni 782.2, Euro milioni 26, na Dola za Canada milioni 2 kutoka kwa washirika wa maendeleo duniani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi na kuongeza ustahimilivu wa sekta mbalimbali.
Hayo yamebainishwa leo Novemba 29, 2024 na Katibu Mkuu Ofisi
ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja katika hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa
Kitaifa kuhusu mrejesho wa ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa 29 wa
Mabadiliko ya Tabianchi (COP29), uliofanyika Novemba 11 hadi 22, 2024 Baku,
Azerbaijan.
Akifungua mkutano huo
kwa niaba ya Katibu Mkuu, Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Bi.
Kemilembe Mutasa amesema sanjari na hilo, pia mashirika na taasisi 30 zimeonesha nia ya kushirikiana na
Tanzania katika miradi ya maendeleo, hususan katika biashara ya kaboni na
juhudi za kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi.
Amesema Mkutano wa COP29 umekuwa wa kihistoria na fursa kwa
Tanzania kwa kuzingatia matokeo na masuala yaliyofikiwa katika mkutano huo
yakiwemo kuanza kufanya kazi rasmi kwa Mfuko wa Kushughulikia Hasara na Upotevu
unaosababishwa na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Hatua hiyo imewezesha kufikiwa kwa lengo la kukusanya shilingi
bilioni 300 kila mwaka hadi mwaka 2035 kutoka shilingi bilioni 100 kwa mwaka na
kukamilishwa na kupitishwa kwa utaratibu wa biashara ya kaboni chini ya Kifungu
cha 6 cha Mkataba wa Paris jambo ambalo linatoa fursa ya kipekee kwa Tanzania.
Aidha, Bi. Kemilembe amebainisha kuwa Tanzania iliingia katika
mkutano huu ikiwa na ajenda na misimamo yake thabiti kuhusu Nishati Safi ya
Kupikia na kusisitiza umuhimu wa kuboresha mazingira kwa kupunguza utegemezi wa
nishati zisizo salama za kupikia kama kuni na mkaa.
“Tulitoa wito wa kuongeza juhudi za pamoja ili kupunguza
gesijoto duniani na kufanikisha lengo la kudhibiti ongezeko la joto duniani
kuwa chini ya nyuzi joto 1.5 ifikapo mwaka 2030.
“Pia, Tanzania ilipata fursa ya kuonesha mafanikio ya
utekelezaji wa hatua mbalimbali za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi
nchini. Juhudi hizi zinajumuisha miradi katika sekta za nishati, kilimo, uchumi
wa buluu, na maji, pamoja na mipango mingine inayolenga kuhimili athari za mabadiliko
ya tabianchi,” amefafanua Mkurugenzi Kemilembe.
Wakiachangia wakati wa mkutano huo, baadhi wa washiriki wa COP29
wameishukuru na kuipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuratibu kwa ufanisi
ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo.
No comments:
Post a Comment