Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) akitoa mkono wa pongezi kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Ikona, Elias Chama (wa pili kulia) mara baada ya kuzindua Barabara yenye urefu wa kilomita 22 katika hifadhi hiyo Kata ya Ikoma, Wilayani Serengeti, Mkoani Mara leo Novemba 15,2024. Wengine pichani ni Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Ikona, Yusuph Manyanda (kushoto), na Mbunge wa Serengeti, Mhe. Dkt.Amsabi Mrimi(wa pili kulia) na na baadhi ya viongozi wa Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Ikona.
Na Happiness Shayo - Serengeti.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amezindua miradi ya kuendeleza utalii ikiwemo Mradi ya Barabara ya Utalii km22 uliogharimu takribani 761.3 na Mradi wa ujenzi wa Vituo Viwili vya kupokea na kukagua wageni(Ikona Gate na Visitors Gate) uliogharimu takribani shilingi milioni 143.5 katika Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Ikona iliyopo Wilaya ya Serengeti Mkoani Mara.
Uzinduzi huo umefanyika leo Novemba 15,2024 katika Jumuiya ya Hifadhi ya Ikona Serengeti Mkoani Mara.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Mhe. Chana ameitaka jumuiya hiyo kuisimamia na kuitumia vyema miradi hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa ya kukuza utalii huku akisisitiza maadili katika utendaji kazi.
"Natoa rai kwa Wafanyakazi kuwa waadilifu katika kutekeleza majukumu ya ulinzi na uhifadhi wa rasilimali za Taifa" amesisitiza Mhe. Chana.
Aidha,
ameipongeza Menejimenti na Jumuiya ya Ikona huku akitoa rai kuendelea
kushirikiana kwa karibu na Halmashauri za Wilaya, Mamlaka ya Usimamizi wa
Wanyamapori Tanzania (TAWA) na Wizara ya Maliasili na Utalii katika kutekeleza
majukumu yao.
Naye, Mhasibu wa Jumuiya ya Ikona, Mariam Magessa amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa Jumuiya hiyo, imefanikiwa kupunguza matukio ya ujangili hivyo kupelekea ongezeko la wanyamapori huku ikivutia shughuli za utalii na wawekezaji.
"Matokeo chanya ya uhifadhi yamepelekea kupata jumla ya wawekezaji 9 ambapo 8 wamewekeza kwenye utalii wa picha na mmoja kwenye utalii wa uwindaji" amesisitiza Mariam na kusema kuwa hiyo imekuwa ni sehemu ya mapato ya Jumuiya hiyo.
Jumuiya ya Ikona
ilianzishwa mwaka 2005 kwa dhumuni la kuendeleza uhifadhi na Usimamizi endelevu
wa Maliasili na vivutio vya utalii kama njia ya kukuza uchumi na hivyo
kupunguza kiwango cha umaskini kwa wananchi wanaoishi katika
vijiji wanachama.
No comments:
Post a Comment