Habari za Punde

Serikali itaendelea kuchukua juhudi maalum kuhakikisha inapunguza kasi ya ongezeko la Maradhi yasiombukiza hapa nchini

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwahutubia Wanamichezo wa Vikundi vya Mazoezi ya Viungo Zanzibar, baada ya kumalizika kwa Matembezi ya Afya Zanzibar “Chagua Mazoezi kuwa Sehemu ya Maisha Yako” yaliyofanyika leo 8-12-2024, katika viwanja vya Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi “B” Unguja na kumalizika katika Uwanja wa Mao Zedung Wilaya ya Mjini Unguja

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk, Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itaendelea  kuchukua juhudi  maalum  kuhakikisha inapunguza kasi ya ongezeko la Maradhi yasiombukiza hapa nchini

Rais Dk,Mwinyi  ametoa tamko hilo alipozungumza  baada ya Kuongoza matembezi ya Afya  yalioandaliwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Taasisi ya Pharm  Access ikiwa ni kampeni maalum ya kudhibiti Maradhi yasioambukiza  kwa jamii  yalioanzia Kiembe Samaki kwa Boutros hadi Uwanja Mao Tse Tung Wilaya ya Mjini.

Rais Dk,Minyi amefahamisha kuwa Tafiti zimeonesha kuwa  Mazoezi yanasaidia kwa kiasi kikubwa  kujenga Afya ya  Mwili ,afya ya akili  na kuondosha Msongo wa Mawazo na kusisitiza jamii kuwa na utaratibu wa kufanya mazoezi kila siku

Aidha Dk, Mwinyi  ameeleza kuwa  Takwimu za  Wizara ya Afya  zimeeleza kuwa  kuna Ongezeko la Maradhi Yasioambukiza kwa kiwango kikubwa ikwemo Kisukari, Presha , Uzito na Unene uliopitiliza na shinikizo la damu kunakosababishwa na  watu wengi kutofanya mazoezi.

Rais Dk, Mwinyi ameeleza kuwa  kutofanya Mazoezi kwa Wananchi walio wengi  kunarejesha nyuma juhudi za Serikali za  kudhibiti Maradhi hayo  na  kupunguza kasi ya kuleta Maendeleo.  

Aidha Rais Dk,Mwinyi amesisitiza kuwa Serikali imeendelea  kushirikiana na taasisi za  Afya  kutoa Elimu na kuhamasisha jamii kutambua umuhimu wa kufanya mazoezi  kwa ajili ya kuimarisha afya zao.

Amefahamisha kuwa Mazoezi yanasaidia kuondoa Msongo wa Mawazo , kuimarisha Usingizi na kuleta furaha.

Ameeleza kuwa  wizara ya Afya  imeendelea kutoa matibabu  bora katika Vituo 60 viliopo Unguja na Pemba   na Kuwasisitiza wananchi kuvitumia Vituo hivyo kupata ushauri wa Kitaalamu wa afya zao.

Rais Dk, Mwinyi ametoa wito kwa  kila mmoja kuchukua hatua ya  kupunguza Mafuta na matumizi ya vyakula vya wanga  kukabiliana na maradhi hayo.

Ameeleza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya  kwa  kushirikiana na  Taasisi Gez Health Initiative  inaendelea kutoa Elimu ,kufanya  Uchunguzi wa Awali wa Maradhi ya Saratani  kupitia Mradi wa miaka mitano wa kudhibiti Saratani  pamoja na  Ujenzi wa kituo cha Umahiri  cha  Saratani  hapa Zanzibar.

Rais Dk, Mwinyi ameshauri kuendelezwa na kupangiwa Utaratibu mzuri  wa  Matembezi ya pamoja  na mazoezi .

Aidha Amezipongeza Taasisi mbalimbali zinazoshirikiana na  Serikali kufanikisha juhudi za Kudhibiti Maradhi yasioambukiza

Waziri wa Afya Nassor Ahmed Mazrui  amesema Dhamira ya Serikali ni kuona wananchi wote  wana afya njema  na kutambua kuwa suala la kufanya mazoezi sio anasa  na  Wizara najiandaa kuwa na siku maalum ya mazoezi kila mwezi.

Ametoa rai kwa Taasisi za Umma na binafsi kuandaa utaratibu wa kuwa na siku maalum ya kufanya mazoezi.

Mkurugenzi wa  Pharm Access Kheri Marwa ameeleza kuwa  tatizo la Maradhi yasioambukiza ni kubwa duniani kote hivyo juhudi kubwa zinapaswa kuchukuliwa kuhamasisha ufanyaji wa mazoezi  kwa wananchi.

Matembezi hayo ya Afya yamebeba Kaulimbiu inayosema "Chagua Mazoezi kuwa Sehemu ya Maisha ".

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.