RAIS wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameiagiza timu kuu ya
kitaalamu ya Dira ya Maendeleo ya 2050 kukutana na wadau mbalimbali kuhakikisha
kazi ya kupokea maoni inakamilika kikamilifu ili kuwa na Dira yenye kubeba
maono ya wananchi wote.
Pia, Dk. Mwinyi ameziagiza Tume za Mipango ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Serikali ya Mapiduzi ya Zanzibar kuhakikisha wanaratibu zoezi la uhakiki kwamba
linafanyika kwa ufanisi wa hali ya juu pamoja na kuisambaza rasimu hiyo kwa vyombo
mbalimbali na kuweka mfumo halisi wa kupokea maoni.
Dk. Mwinyi ameyasema hayo alipozindua Rasimu ya Dira ya Taifa
ya Maendeleo 2050, hotel ya Golden Tulip Uwanja wa ndege Mkoa wa Mjini
Magharibi, hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali za SMT na
SMZ akiwemo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaaliwa na
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi
amewaagiza viongozi na wataalamu wote wa Serikali zote mbili kutoa ushirikiano
kwa timu ya kitaalam ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwani kutoshiriki kwao
hakutofanikisha azma ya Dira hiyo.
Rais Dk. Mwinyi pia ameisisitiza timu hiyo ya
Kitaalam kuhakikisha inamfikia kila mwanchi kote nchini ili kutoa maoni bila
kujali tofauti za dini, siasa, jinsia, makundi maalum au eneo mtu analotoka
kwani Raisimu hiyo ni ya Watanzania wote, hivyo alieleza ni lazima ibebe maono
yao ya miaka 25 ijayo.
Dk. Mwinyi amebainisha malengo makuu ya Rasimu hiyo
ni kuona yamegusa
moja kwa moja katika kuboresha maisha ya watu, elimu, afya, ustawi wa amani na haki
pamoja na kuwa na Dira jumuishi ambayo itamshirikisha kila mwananchi kutoa
mchango wake kwa maendeleo ya Taifa.
Ameishauri timu hiyo kuweka muktadha wa maendeleo ya Taifa katika mwelekeo
wa makubaliano au mipango ya kikanda na kimataifa, akitolea mfano “Dira ya Maendeleo ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki” (EAC) 2050; “Dira ya Jumuiya ya Maendeleo
Kusini mwa Afrika” (SADC) 2050; “Makubaliano ya Paris kuhusu
Mabadiliko ya Tabianchi” (Paris Agreement); “Ajenda ya Maendeleo ya Afrika” (Ajenda 2063); “Doha Programme of Action 2022 –
2023” na
Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 (SDGs)
Aidha, Rais Dk. Mwinyi
ameishauri timu hiyo ya kitaalamu kuandaa usimamizi mzuri wa kukusanya maoni ya
wadau kwa kuzunguka nchi nzima na kuandaa makongamano na majadiliano na wadau.
Akitaja mafanikio ya
Dira ya 2025 ambayo inafikia tamati
mwezi Juni 2025, amesema kuwa ni pamoja na Kuboresha hali ya Maisha ya watu,
elimu, Uboreshaji wa huduma za afya, kupunguza vifo na kuongezeka wastani wa
umri wa kuishi, kuimarika kwa utawala wa kisheria na ukuaji wa uchumi.
Alisema, kwa kipindi
chote cha utekelezaji wa Dira 2025, nchi imekuwa kitovu cha amani na imeshiriki
kikamilifu hata katika duru za kimataifa kulinda amani barani Afrika,
aliwasisitiza Watanzania kuendelea kulinda amani, utulivu na umoja kama misingi
muhimu ya kupata maendeleo ya nchi.
Ameeleza kuwa Tanzania ni
miongoni mwa nchi chache zenye utoshelevu wa chakula kwa asilimia 124. Licha ya
kuwa bado kilimo hakijawa cha kisasa, lakini wakulima wamefanya kazi kubwa ya
kuhakikisha nchi haikabiliwi na njaa.
Akizungumzia ustawi wa Elimu
amesema kumeshuhudiwa ongezeko kubwa la madarasa, vyuo vikuu na walimu. Aidha,
udahili wa elimu ya msingi umeongezeka kutoka 69% kutoka mwaka 2000 hadi
kufikia 97% mwaka 2022, kuongezeka kwa kiwango cha kumaliza elimu kutoka 51%
mwaka 2000 hadi 70% mwaka 2022 na kufanikiwa kuondoa pengo kubwa lililokuwepo
katika elimu ya msingi na sekondari kati ya watoto wa kike na watoto wa kiume.
Aidha, kuimarisha
kiwango cha ufaulu katika mitihani ya darasa la saba kutoka 22% mwaka 2000 hadi
kufikia 80% mwaka 2022; kuongezeka kwa kiwango cha kujiunga na elimu ya
sekondari kutoka 20% hadi 70%; na ongezeko la wanafunzi wanaopata elimu ya juu
kutokana na Serikali kuongeza fedha za mikopo ya elimu ya juu. Hatua hiyo imefikiwa kutokana na Serikali
kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha katika sekta ya elimu kwa kuzingatia umuhimu
wake katika kuchochea maendeleo ya nchi yetu.
Kuhusu Uboreshaji wa huduma za afya alisema Dira 2025 ilifanikiwa
kupunguza vifo na kuongezeka wastani wa umri wa kuishi, kuimarika kwa hizo
kuanzia kwenye vituo vya fya, zahanati, hospitali za wilaya, mikoa, kanda hadi Taifa.
Akielezea Utawala bora
na utawala wa sheria ameeleza kuwa limebaki kuwa kipaumbele kwa Taifa licha ya
changamoto ndogo ndogo ambazo zimeendelea kushughulikiwa na Serikali kwa
masilahi mapana ya wananchi ikiwemo kuundwa kwa Tume ili kupendekeza namna ya
kuboresha Taasisi za Haki Jinai nchini ikiwa ni njia ya kuendelea kuimarisha
zaidi mifumo ya haki jinai na hivyo kudumisha utawala bora na utawala wa
sheria.
Hata hivyo ameweleza
mafanikio ya uchumi wa nchi umekuwa kwa wastani wa 6.7% ikiweko kukua kwa biashara
na uwekezaji, kujenga miundombinu muhimu kwa sekta zote ikiwemo ujenzi wa barabara
na madaraja makubwa, reli ya kisasa, ukarabati mkubwa wa reli ya kati, bandari,
meli, viwanja vya ndege, miundombinu ya mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.
Akizungumza katika hafla
hiyo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaaliwa amsema
uzinduzi wa rasimu ya 2050 ni jambo kubwa lenye mustakabali muhimu kwa Taifa la
Tanzania.
Amebainisha kuwa Raismu
hiyo ni ya Watanzani wote na kuahidi timu ya kitaalamu ya Dira hiyo kuendelea
kutekeleza majukumu yake kwa weledi na uaminifu ili hatimye kuwa na Dira ya
2050 yenye tija na manufaa kwa Watanzania.
Naye, Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya
Uongozi ya Kitaifa ya Maandalizi ya Dira
2050, Prof. Kitila Mkumbo, ameleza msingu mkuu wa Rasimu hiyo umejikita katika
usalama, amani na utulivu na kuwa na uchumi imara. Pia ameeleza uzinduzi wa
Rasimu hiyo ni mwanzo wa safari na hatimaye itawasilishwa Bungeni kwaajili ya
mijadala.
Kwa upande wake Dk.
Saada Mkuya Salum, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Fedha na Mipango wa Zanzibar
na Makamu Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Uongozi ya Kitaifa ya Maandalizi ya Dira 2050,
Zanzibar imeshiriki kikamilifu kutoa maoni juu ya rasimu hiyo kwa hatua
mbalimbali ikiwemo kuratibu maoni ya wananchi huku kukiwa na ushiriki mkubwa wa
wanawake.
Rais Dk. Mwinyi
alikabidhi Rasim ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 kwa Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaaliwa kwa niaba ya Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe.
Hemed Suleiman Abdulla kwa niaba ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Pamoja na Watendaji wa kuu wa Taasisi za Umma
na binafsi.
IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment