Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana Zanzibar, Shaib Ibrahim Mohamed, Mratibu kutoka Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani, (Save the Childen) Barnabas Kaniki na Mratibu kutoka Tanzania Bora Initiative, , Alfred Kiwuyo pamoja na Maafisa wa Wizara hiyo katika hafla fupi ya kuutambulisha Mradi wa Vijana Plus huko Migombani, Wilaya ya Mjini.
Imetolewa na Kitengo cha Habari,Mawasiliano na Uhusiano.
Na.Khadija Khamis , WHVUM.
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana Zanzibar, Shaib Ibrahim Mohamed amelishukuru Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani, Save the Childen na Tanzania Bora Initiative, kwa uwasilishaji wa mradi wa Vijana Plus ambao utawafikia makundi mbali mbali ya vijana wa Zanzibar.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana,Utamaduni na Michezo Ndugu Fatma Hamad Rajab katika hafla fupi ya utambulisho wa mradi wa ‘ Vijana Plus’ katika ukumbi wa Wizara hiyo Migombani Wilaya ya Mjini.
Amesema mradi huo utasaidia kuwajengea uwezo vijana katika usimamizi na utekelezaji wa mashirika yao ili kuepukana na changamoto zinazowakwamisha katika uimarishaji wa maendeleo yao.
Aidha amewaomba mashirika hayo kuendeleza mashirikiano yao na Wizara ya Habari, Vijana Utamaduni na michezo ili kuhakikisha mradi huo unatekelezwa ipasavyo na kuleta tija jambo ambalo litasaidia kuimarisha ustawi na maendeleo ya vijana Wazanzibar.
Amesema Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo inaratibu na kusimamia maendeleo ya vijana, utekelezaji wa maendeleo hayo hutekelezwa na wadau mbali mbali wa sekta za Serikali, Sekta Binafsi pamoja na wadau mbali mbali kutoka ndani na nje ya nchi, Wizara inatambua uwepo wao kwa mujibu wa Sera ya Maendeleo ya Vijana ya Mwaka 2023.
Nae Mtaalamu wa Ulinzi na Utawala wa Haki za Watoto kutoka Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani, (Save the Childen) Barnabas Kaniki amesema lengo la mradi wa Vijana Plus ni kuyawezesha mashirika ya Vijana na viongozi wake kuwa wadau wakuu kwenye masuala ya utawala bora na maendeleo.
Amefahamisha kuwa vijana watakaolengwa kupatiwa fursa hiyo katika mradi huo ni kati ya umri wa miaka 15 hadi 29 katika kanda mbali mbali iliyopangiwa ikiwemo Dodoma , Mwanza , Tanga, Zanzibar, Mtwara, Mbeya, Kigoma pamoja na Morogoro.
Ameeleza kuwa mradi huo utawajengea uwezo vijana wa mashirika 40 kwa kuzitatua changamoto zilizopo na kuwapa elimu viongozi wao 100 kutoka katika mashirika hayo ili kuwajengea uwezo kiufanisi.
Kwa upande wa Mratibu wa Mradi kutoka Tanzania Bora Initiative, Alfred Kiwuyo amesema anatarajia mradi huo utawafikia vijana wengi ambao bado hawajawahi kufikiwa ili kufikia lengo lililokusudiwa kwa kuwafungulia njia za kimaendeleo.
Amesema makongamano mbali mbali yatafanyika ili kuwapa fursa vijana wa sekta tofauti mashirika na makundi mbali mbali ikiwemo wajasiriamali,wasanii pamoja na waandishi wa habari ili kuwaengezea ujuzi katika maeneo wanayofanyia kazi.
Mradi wa Vijana Plus ni wa miaka mitatu ulianza mwaka 2025 hadi 2028 unaotarajiwa kuwafikia vijana wa kitanzania 711,880 ikifadhiliwa na Save the Childen wakishirikiana na Tanzania bora Initiative, mradi huo umewekwa Bajeti ya Auro Milioni 2.2 .
No comments:
Post a Comment