Habari za Punde

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Alhajj Kasim Majaliwa Azindua Mskiti wa Masjid Nuuril Hikma Yombo Temeke Jijini Dar es Salaam

Muonekano  wa msikiti wa Jaami'u Nuuril Hikma uliopo Yombo, Temeke jijini Dar es salaam amber Waziri Mkuu, Kasssim Majaliwa aliuzindua  Machi 14, 2025.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kuzindua msikiti wa Jaami'u Nuuril Hikma uliopo Yombo, Temeke jijini Dar es salaam, Machi 14, 2025.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikata utepe kuzindua msikiti wa Jaami'u Nuuril Hikma uliopo Yombo, Temeke jijini Dar es salaam, Machi 14, 2025. Kushoto kwake ni  Rais wa Taasisi ya Alhikma, Shareef Abdulqadir Al-ahdal na kulia kwake ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa Mstaafu, Abdulrahman Kinana.
 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizundua msikiti wa Jaami'u Nuuril Hikma uliopo Yombo, Temeke jijini Dar es salaam, Machi 14, 2025. Kushoto ni  Rais wa Taasisi ya Alhikma, Shareef Abdulqadir Al-ahdal. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

 

* Awataka waumini kuutunza msikiti huo

* Atoa wito kwa viongozi wa dini kuliombea Taifa na kukemea maovu

 

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa leo Machi 14, 2025 amezindua msikiti wa Masjid Jaami’u Nuuril Hikma uliopo mtaa wa Yombo, Temeke jijini Dar es Salaam ambao umejengwa na Taasisi ya Al-Hikma

 

Akizungumza baada ya kuzindua msikiti huo, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa jamii na Watanzania watakaotumia msikiti huo kuutunza kwani kufanya hivyo ni njia ya kudumisha uhusiano na Mwenyezi Mungu na inahesabika kama sadaka.

 

“Mtume Muhamad S.A.W anatufundisha pia kutunza nyumba za ibada, msikiti ni sehemu ya jamii na ni mahali pa ibada na umoja. Kupitia hadithi ya Bukhari, ni wajibu wa waumini kutunza msikiti, kuhakikisha kwamba ni sehemu safi, na inakidhi mahitaji ya ibada na mafunzo ya kiislamu.”

 

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa msikiti ni kituo cha kiroho, kijamii, kiutamaduni na nyumba kwa ajili ya ibada na unatoa nafasi kwa waumini kushirikiana katika ibada, kujifunza, na kujenga jamii bora kwa kutoa huduma za kijamii.

 

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa viongozi wa dini kuliombea Taifa pamoja na kukemea vitendo vyote visivyo mpendeza Mwenyezi Mungu.

 

“Tunajua mnaliombea Taifa hili, ila endeleeni kufanya hivyo ili utulivu huu uendelee, tuachane na mambo yatakayoleta adha kwenye jamii, tunafurahi mnavyohubiri amani na mshikamano, Mwenyezi Mungu analipenda Taifa hili.”

 

Kwa upande wake Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Sheikh Dkt Abubakar Zuber Ali Mbwana amesema kuwa maendeleo sio ugomvi bali ni kufanya mambo yanayoonekana na  yanayompendeza Mwenyezi Mungu ikiwemo ujenzi wa msikiti “fitna, ugomvi, fujo kwenye misikiti hatutaki, tupendane na heshima itawale.” 

 

Pia Mheshimiwa Majaliwa ameipongeza Taasisi ya Al-Hikma kwa ujenzi wa msikiti huo. “Ujenzi wa Msikiti huu ni ishara ya juhudi za taasisi hii katika kuimarisha misingi ya imani na maadili mema katika jamii”.

 

Kwa upande wake Rais wa Taasisi ya Alhikma Shareef Abdulqadir Al-ahdal amesema kuwa imekuwa faraja kwao kufanikiwa kukamilisha ujenzi wa msikiti huo. “Furaha yetu ni kuona tumekamilisha ujenzi wa msikiti huu ambao ni wa waislam wote na sio wa mtu mmoja.”

 

Msikiti huo ulioanza kujengwa Aprili 21, 2022 na kukamilika Machi 07, 2025 ni wa gorofa nne na unauwezo wa kuingiza waumini 3,200 kwa wakati mmoja.

 

(mwisho)

 

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

S. L. P. 980,

41193 – DODOMA.

IJUMAA, MACHI 14, 2025.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.