Habari za Punde

ZAECA Yatoa Elimu ya Rushwa kwa Watumishi wa Umma

Mkurugenzi Idara ya Utumishi na Uwendeshaji katika Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Rashid Hamdu Makame amesema elimu iliotolewa na Mamlaka ya kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi (ZAECA), itawasaidia Wafanyakazi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Ameyasema hayo wakati alipokuwa akifunguwa Mafunzo ya kuwajengea uwelewa Wafanyakazi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, kuhusiana na masuala ya Rushwa na Uhujumu uchumi huko Migombani Wilaya ya Mjini.

Amewataka Wafanyakazi hao, kuzingatia kwa makini mafunzo hayo kwa kuepukana na madhara ya kutoa na kupokea rushwa ili kufikia malengo ya Serikali kutokomeza Rushwa Nchini.

Akiwasilisha mada ya Rushwa na Uhujumu wa Uchumi, Afisa Elimu kwa Umma kutoka ZAECA Saada Salum Issa amesema lengo la kutoa elimu hiyo, ni kukuza mashirikiano katika Taasisi za Serikali, binafsi na jamii kwa ujumla ili kuimarisha  uadilifu na utendaji wa kazi.

‘’Kutojua Sheria sio sababu ya kutokuwa na hatia, ninawasihi wafanya kazi wenzangu tujitahidi sana kujiepusha  na masuala ya Rushwa ni hatari ‘’alisema Afisa huyo.

Aidha amewataka Wafanya kazi kujikinga na madhara mbalimbali yanayoweza  kupatikana ikiwemo kifungo, kusimamishwa kazi pamoja na faini.

Akitaja baadhi ya makosa amesema kuwa ni pamoja na matumizi mabaya ya madaraka, uhaulishaji wa Mapato, Rushwa ya Ngono, Utakasishaji wa Fedha, Rushwa ya Zabuni na Udanganyifu wa aina yoyote.

Kwa upande wa Mkuu wa Devisheni ya Utumishi katika Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Subira Mtumwa Haji amesema mafunzo hayo ni muhimu na amewashauri Watendaji kuyazingatia ili kuepukana na matatizo yanayoweza kujitokeza.

IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI

WHVUM

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.