Habari za Punde

Majaliwa : Sherehe za Muungano za Mwaka huu Zifanyike Mokoa Yote

 *Viongozi wa Serikali kuongoza, rai yatolewa  kwa wananchi washiriki       kikamilifu

*Ampongeza Rais Dkt. Samia kwa kuifungua nchi kwenye nyanja za kidiplomasia

 

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza maadhimisho ya sherehe za Muungano za mwaka huu yafanyike katika mikoa yote yakiongozwa na viongozi wakuu wa Serikali.

 

Ameyasema hayo jana (Jumatano, Aprili 9, 2025) alipowasilisha hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Mtumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2025/2026 Bungeni jijini Dodoma.

”Viongozi hao pamoja na masuala mengine, watajumuika na wananchi katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo uzinduzi wa miradi ya maendeleo. Nitoe rai kwa wananchi wote kushiriki katika maadhimisho hayo yatakayofanyika tarehe 26 Aprili ili kuendelea kuenzi Muungano wetu.”

 

Mheshimiewa Majaliwa alisema Serikali imeendelea kuratibu vikao vya kamati ya pamoja kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ajili ya kushughulikia masuala ya Muungano.

 

Alisema katika mwaka 2025/2026 Serikali itahakikisha kwamba hoja za Muungano zilizopo na zitakazojitokeza zitashughulikiwa kikamilifu. Vilevile, itaendelea kutekeleza miradi na programu mbalimbali za maendeleo kwa lengo la kuudumisha na kuulinda Muungano huo.

 

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema uhusiano kati ya Tanzania na nchi nyingine, jumuiya za kikanda na kimataifa umeendelea kuimarika na nchi yetu imeendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika kutekeleza majukumu ya kidiplomasia.

 

Alisema katika mwaka 2024/2025, Serikali imeshiriki kikamilifu katika shughuli za kimataifa ikiwemo Mkutano wa Wakuu wa Nchi Tajiri Duniani za Kundi la G20 uliofanyika Rio de Janeiro, Brazil; Mkutano wa 29 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabia Nchi (COP 29).

 

Mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa uliofanyika New York nchini Marekani;  Mkutano wa 27 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola (CHOGM 2024); Mkutano wa 46 wa Kamati ya Urithi wa Dunia ya UNESCO uliofanyika New Delhi, India na Mkutano Mkuu wa 68 wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomu (IAEA), uliofanyika Vienna, Austria.

 

”Nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ni mwanadiplomasia namba moja nchini kwa kutoa kipaumbele cha kuifungua nchi kwenye nyanja za diplomasia ya kiuchumi na kisiasa katika medani za kimataifa.”

 

Alisema katika mwaka 2025/2026 Serikali itaendelea kuratibu ziara za kimkakati za viongozi wakuu wa kitaifa nje ya nchi, na ziara za viongozi wakuu wa mataifa mengine pamoja na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa hapa nchini.

 

 (mwisho)

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,                    

ALHAMISI, APRILI 10, 2025

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.