Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla Amefungua Mkutano wa AGN

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewataka washiriki wa Mkutano wa kundi la majadilano la Afrika kuhusu mabadiliko ya Tabianchi kuhakikisha mijadala yao inalenga zaidi kuangalia fursa na changamoto ambazo Afrika inakabiliana nazo pamoja na kuweka vipaombele muhimu vya kimkakati vitakavyo isaidia  Afrika kupambana na mabadiliko ya Tabianchi.

Ameyasem ahayo  kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt  Philip Isdori Mpango  katika ufunguzi Mkutano wa Kundi la majadilano la Afrika (AGN) unaohusu  mabadiliko ya Tabianchi uliofanyika katika Ukumbi wa Hotel Verde Mtoni jijini  Zanzibar.

Amesema Mkutano huo ni muhimu sana kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla ambao utajadili mambo mbali mbali ikiwemo matumizi ya nishati safi ya kupikia pamoja na kuwaunganisha waafrika zaidi ya milioni 300 katika matumizi ya nishati safi ifikapo mwaka 2030 ili kuweza  kuhifadhi mazingira na kukabiliana na  mabadiliko ya tabianchi Barani Afrika.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amefahamisha kuwa  muelekeo wa udhibiti wa mabadiliko ya tabianchi Barani Afrika ni mzuri na  kwa upande wa Tanzani wananchi wananuwelewa wa kutosha juu ya matumizi ya nishati safi ambapo matarajio ya Serikali ni kuona  watanzani wote wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2030.

Mhe. Hemed amesema athari za mabadilko ya hali ya hewa zimekuwa zikiongezeka na nchi nyingi za Afrika zimekuwa zikikabiliwa na athari mbaya kutokana na kupungua kwa fedha za hali ya  hewa jambo lililopelekea wazalishaji wakubwa wa hewa kujiondoka kutokana na changamoto hio.

Aidha, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amefahamisha kuwa licha ya Bara la Afrika kuwa na utajiri wa asili kama vile kuwepo kwa madini muhimu kwa Teknolojia ya kijani kibichi lakini bado zaidi ya Waafrika milioni 600 hawana uwezo wa kupata nishati safi na nafuu kama vile nishati ya kupikia jambo ambalo halikubaliki ambapo  jitihada za haraka zinapaswa kuchukuliwa ili kukabiliana na changamoto hio.

Makamu wa Pili wa Rais  wa Zanzibar amefahamisha kuwa Afrika inapaswa kutumia rasilimali zake ili kuvutia wawekezaji hasa  katika nishati ya kijani na Teknolojia zinazosukuma maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Sambamba na hayo Mhe.Hemed amewataka washiriki wa mkutano huo kuangalia namna bora za udhibiti na uhifadhi wa mazingira kupitia mikataba na miongozo mbali mbali ya Kimataifa ambayo itainufaisha zaidi Bara la Afrika katkak suala zima la Mazingira.

Nae Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar Mhe. Harusi Said Suleiman amesema kufanyika kwa mkutano huo kunaonesha umuhimu unaowekwa na AGN katika kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi na kuhakikisha kuwa Afrika iko salama kimazingira.

Mhe.Harusi amesema mkutano huo una lengo la kuimarisha na kufanya  ushawishi kwa nchi za Afrika katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuweka mikakati na maadhimio thabiti  yenye kuisaidia Afrika kuepukana na changamoto mbali mbali za kimazingira na kuweza kufika malengo waliyojiwekea .

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mkutano wa kundi la majadiliano la  Afrika kuhusu mabadiliko ya Tabianchi ( AGN ) Dkt. Richard Muyungi amesema mkutano huo utajadili na kutoa maamuzi juu ya masuala ya tabianchi jinsi  yatakavyoshughulikiwa kwa mwaka mzima pamoja na mambo mengine ya msingi ambayo Afrika inataka yasimamiwe katika kuelekea mkutano mkubwa wa nchi zote duniani na mkataba wa  mabadiliko ya tabianchi.

Dkt. Muyungi amesema mkutano huo utazingatia  mambo muhimu ikiwemo kuweka mikakati ya kupunguza gesi joto na kuongeza uvumilivu wa mabadilo ya tabianchi pamoja na kuhakikisha Afrika inatumia nishati za mpito ambayo itaipeleka Afrika katika dunia iliyo salama sambamba na kuachana kabisa na matumizi ya nishati za mafuta lengo ni kuhakikisha Afrika inalinda na kuhifadhi mazingira.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
Tarehe 28.04.2025

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.