Habari za Punde

MAKAMU WA PILI WA RAIS ZANZIBAR- KUWASILI MKOANI MTWARA KWA SHUGHULI ZA KIKAZI

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla akiwasalimia wananchi wa Mkoa wa Mtwara mara baada ya kuwasili Mkoani humo kwa shughuli mbali mbali za kikazi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla amewataka Viongozi na watendaji wa Mkoa wa Mtwara kuendelea kuwatumikia wananchi Mkoni humo na Mikoa jirani kwa kuzingatia misingi ya sheria na uadilifu wa hali ya juu.

Ameyasema hayo wakati akipokea taarifa ya utendaji kazi wa mkoa wa Mtwara  katika ukumbi wa Hoteli ya Genesis mara baada ya kuwasili mkoani humo kwa ajili ya shughuli za kikazi ikiwemo maadhimisho ya  miaka 61 ya muungano wa Tanganyika na zanzibar.

Amesema adhma ya Rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan ni kuona Wafanyakazi wanawajibika ipaswavyo kulingana na nafasi zao kwa kuzingatia misingi ya sheria, haki na usawa katika kutekeleza majukumu yao ya kuwatumikia Watanzania.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema Mkoa wa Mtwara umepata mafanikio makubwa chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia ikiwemo kutanuliwa kwa Bandari, ujenzi wa skuli na madarasa, vituo vya Afya, miundombinu ya maji na barabara na huduma mbali mbali za kiuchumi na kijamii mkoani humo zimeimarika.

Aidha, Mhe. Hemed amefahamisha kuwa Tanzania ni nchi inayoongozwa kwa kufuata misingi ya kidemokrasia na miongozo iliyowekwa kwa makubaliano katika kuhakikisha Tanzania inazidi kuimarika kimaendeleo.

Sambamba na hayo amewataka wananchi wa Mtwara na Tanzania kwa ujumla kuitunza amani, mshikamano na utulivu uliopo nchini pamoja na kuulinda na kuudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao ndio chachu ya maendeleo yaliyopo nchini.

Akitoa salamu za Mkoa wa Mtwara Mkuu wa Mkoa huo Kanal PATRIC KENANI SAWALA ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita(6) kwa kuufanya mkoa wa Mtwara kuwa ni miongoni mwa mikoa ya kimkakati kwa kuekeza katika miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwemo utanuzi wa bandari ya Mtwara, ujenzi wa skuli, vituo vya afya  pamoja na miundombinu ya barabara ambayo inawasaidia wakulima na wafanyabiashara  Mkoani  huo kusafirisha mazao na kuuza mikoa jirani kwa urahisi zaidi.

Kanal PATRIC amesema kutokana na kuimarika kwa miundombinu Mkoani humo kumepelekea kukuwa kwa uchumi na kuongezeka kwa pato la mtu mmoja mmoja na Taifa kupitia shughuli mbali mbali zinazofanywa na wakaazi wa Mtwara ikiwemo kilimo, uvuvi, biashara utalii na nyenginezo jambo lililochangia kupunguza ukali wa maisha kwa wanamchi wa Mkoa wa Mtwara.

Wakati huo huo makamu wa pili wa rais wa zanzibar ambae pia ni mjumbe wa kamati kuu ya halmashauri kuu ya CCM taifa Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ametembelea Ofisi ya Kuu ya CCM Mkoa wa Mtwara na kuzungumza na viongozi mbali mbali wa Chama Cha Mapinduzi Mkoani humo.

Imetolewa na kitengo cha Habari ( OMPR )

Leo tarehe 24 / 04 / 2025

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.