Habari za Punde

DEMOKRASIA SIO RUHUSA YA KUTUKANA WENGINE - WASIRA

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Stephen Wasira amesema siku hizi dunia imeanza kutoa  tafsiri nyingine ya uhuru kwamba mkitukanana sana katika mitandao ya kijamii ndio uhuru lakini ukweli hakuna uhuru usio na mipaka na hakuna uhuru au demokrasi ya kutukana mitandaoni.

*Asema hakuna uhuru wa kutoa maoni wa kutukanana katika mitandao ya kijamii

*Asisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria katika kutoa maoni

*Awakumbusha wana ccm kutenda haki katika vikao vya kuchuja wagombea


Na Mwandishi Wetu

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Stephen Wasira amesema siku hizi dunia imeanza kutoa  tafsiri nyingine ya uhuru kwamba mkitukanana sana katika mitandao ya kijamii ndio uhuru lakini ukweli hakuna uhuru usio na mipaka na hakuna uhuru au demokrasi ya kutukana mitandaoni.

Akizungumza katika kikao cha ndani na viongozi wa Chama hicho Wilaya Songea Vijijini mkoani Ruvuma ,Wasira ametumia nafasi kueleza kwa sasa kumekuwepo ba tabia ambayo si utamaduni wa Watanzania kwani kumeibuka utamaduni wa kuona ni jambo la kawaida kutukanana katika mitandao ya kijamii.

"Lakini hebu  niulize wazee watuambie hivi huku (Songea)katika mila  na utamaduni watoto walikuwa wanatukana baba zao, walizuiwa na nani? Walizuiliwa na utamaduni.Watoto hawakuwa na nafasi ya kumtukana baba wala mama hata kama atakuwa amekosea bali walikuwa wamejiwekea utaratibu tofauti na wa demokrasia ya sasa...

"Mtoto hawezi kusema baba naye amezidi tupige kura kupata baba mwingine, hata akiwa mkorofi wanasema ah! baba naye hata akiwa mlevi wanasema baba naye karudi leo kayanywa lakini hawasemi uongozi wake unakoma wa ubaba, hapo ndipo tulipoanzia,"amesema Wasira .

"Sasa unapopanua demokrasia, tena unapokuja kwenye kitu kipya kinachoitwa vyama vingi vyama vingi vizuri sana lakini na vyenyewe vinaweza kuwa tabu sana, lakini hakuna kisicholuwa na tabu jambo kubwa ni kuweka utaratibu ili vyama hivi vifanye kazi kwa kuzingatia katiba na sheria mliyojiwekea, amesema Wasira.

Amefafanua kuwa uhuru ni kutoa maoni kwa kufuata sheria maana unaweka sheria ambazo zinaifanya jamii iishi pamoja bila ya bughudha ili kuondoa mtu asimuonee mwingine lakini hata kutukana ni kosa la jinai ukisoma sheria za Tanzania.

"Ukitukana mtu hapo Peramiho akikupeleka Polisi ukauliza nini ukasema kanitukana Polisi hawezi kuacha na itabidi ueleze ilikuaje, alisemaje, mlianzaje, sheria.Lakini siku hizi ukisoma mitandao eti matusi ndio demokrasia, eti matusi ndio uhuru ah!

"Uhuru wa kutukanana sasa hapo tumekosea njia , ungekuwa uhuru wenyewe ni wa kutukanana tungeutafuta wa nini? Tulitafuta  uhuru ili utusaidie kujenga watu pamoja na kuleta amani katika  kuleta nchi na kusimamia maendeleo yao."

Akizungumza kuhusu kuelekea uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu, Wasira ameendelea kuwakumbusha viongozi wa Chama hicho ngazi ya Wilaya na Mkoa kutenda haki kwa watakaojitokeza kugombea ubunge au udiwani.

Pia amesema katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wagombea waache mtindo wa kizamani wa kufikiri kwamba wanaweza kushinda nafasi za uongozi kwa kugawa fedha kwa wajumbe au wapigakura.

Wasira alisema hata kama mtu anapendwa kiasi gani hawezi kukosa watu kadhaa wa kumkataa hivyo mchakato wa kuchujwa lazima utazingatiwa, na mgombea atashinda kutokana na kazi yake.

Alifafanua uchaguzi sio ajali, tangu siku ya kwanza mbunge au diwani alipochaguliwa  alikuwa anajua baada ya miaka mitano uchaguzi utakuja, hakuna mtu anayeuzuia wala kuuharakisha, hivyo sasa umefika na kazi ya CCM ni kutazama mazingira yao na kuleta mabadiliko pale ambako yanahitajika.

"Tunatumia mtindo wa mkutando mkuu wa wilaya kupiga kura za maoni kwaajili ya wabunge, sasa idadi ya wajumbe katika mkutano huo wameongezwa  ili kuondeza demokrasia na kuondoa mazingira ya rushwa," alisema.

Alifafanua pia lengo la kuwaongeza wajumbe hao ni ili watakapofanya maamuzi ya kumpendekeza mgombea fulani basi waamini kuwa wananchi watamuunga mkono kutokana na kazi aliyoifanya.

"Kwa maana nyingine tunataka nyie wapigakura za maoni mukisaidie chama chenu kujua nani akigombea anashinda bila tabu, na awe anakubalika sio kujulikana maana hata wezi wanajulikana, awe anakubalika na imani ya wananchi," alisisitiza Wasira.

Pia alisema mchakato huo utawahusu wabunge na madiwani, huku akiwataka wajumbe wa mkutano huo wilaya kupiga kura kwa kuzingatia uwezo wa mgombea, akisisitiza kwamba wasije wakamuonea mtu kama amefanya kazi vizuri apewe fursa ya kuingia kwenye tatu bora ili wananchi wakaamue.

"Lakini kama ulitoroka watu, usije ukasema sasa mimi nimekosa nini umewakosea waliokupa kazi, kwanini uliwatoroka, kuna mbunge aliposikia naenda mahala fulani nae akaja anawaambia wananchi nimerudi nyumbani, wakamuuliza ulikuwa wapi, mbona hukutuaga sisi waajiri wako.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.