Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Aendelea na Ziara yake ya Kichama

Mjumbe wa Kamati Kuu ya  Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema katika maandalizi ya kuelekea uchaguzi mkuu wanachama wa CCM wanatakiwa kusimama pamoja kuhakikisha CCM inashinda kwa kishindo.

Ameyasema hayo alipokutana na Viongozi wa Halmashauri Kuu ya Wilaya, Kamati za Siasa za Jimbo na wadi ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kuimarisha chama ndani ya Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini kichama kwenye Ukumbi wa ZSSF Kariakoo.
Amesema dhamira ya chama chochote cha siasa ni kushinda hivyo umoja, mshikamano na maelewano ya viongozi na wananchama ndio nyenzo pekee ya kuviangusha vyama vya upinzani.

Amewaasa viongozi na wanachama kuacha tabia ya kuchafuana, kufanyiana chuki na  migogoro ndani ya chama jambo ambalo linaweza kuwaumiza baadhi ya watu na kuwakosesha haki zao pamoja na kukiathiri chama kwa utashi wa mtu binafsi .

Amesema wakati umefika kwa wana CCM kuchagua wagombea wenye mapenzi na nia thabiti ya kukitumikia chama na kuweza kuwafikia wananchi majimboni kusikiliza kero zao na kuzifanyia kazi.

Mhe. Hemed amevitaka vikao vya maamuzi kufuata matakwa ya katiba ya chama kwa  kufanya haki na uadilifu wakati wa kupitisha wagombea ili  kuepuka migogoro isiyokuwa ya lazima ndani ya chama na kwenye jamii itakayopelekea mgawanyiko na mipasuko ya wenyewe kwa wenyewe.

Mhe. Hemed amewataka wanachama wa CCM kuendelea kudumisha Amani na Utulivu kwa kipindi chote cha maandalizi ya kuelekea uchaguzi na kuwasihi watakaoteuliwa kugombea nafasi mbali mbali wakafanye kampeni za kistaarabu zenye kuelezea mazuri yanayofanywa na viongozi wa chama na Serikali.

Amewahamasisha  wanawake na vijana kutokubali kukatishwa taamaa kwa kuonekana hawana uwezo wa kuongoza badala yake wajitokeze kwa wingi katika kuchukua fomu na kugombea nafasi mbali mbali.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Ndugu Talib Ali Talib amesema  hakuna jimbo hata moja ndani ya Wilaya ya Mjini litakalochukuliwa na wapinzani kutokana na mipango na mikati madhubuti waliyoiandaa ya kuhakikisha CCM inashinda kwa kishindo.

Talib amewataka wanachama wa CCM wa Mkoa wa Mjini kuhakikisha hakuna kura hata moja ya CCM itakayopotea ifikapo mwezi Oktoba.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mjini Kichama ndugu Hamid Mbwana Said amemuhakikishia Mhe. Hemed kuwa watatenda haki na kuwa waadilifu katika mchakato wote wa kupitisha wagombea na hakutakuwa na ubabaishaji wala figisu figisu ya aina yote ile.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mhe.Hemed Suleiman Abdulla ametamatisha ziara yake ya kuimarisha Chama cha Mapinduzi kwa upande wa Unguja.


Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
Tarehe 17.06.2025

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.