MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema serikali itaendelea kushirikiana kikamilifu na wataalamu wa fani za usanifu, uhandisi, ukadiriaji na teknolojia katika kutekeleza miradi mikubwa ya mikakati nchini.
ameyaeleza hayo kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt Hussein Ali Mwinyi alipofungua mkutano wa pili wa Taasisi ya Wasanifu, Wahandisi na Wakadiriaji Majengo Zanzibar uliofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Verde iliyopo mjini Zanzibar.
Amesema serikali ya awamu ya nane(8) imejikita kwenye miradi ya kimkakati ambayo kwa asilimia kubwa ni ya ujenzi, hivyo wataalam wa fani za usanifu, uhandisi ukadiriaji wana nafasi ya kushirikiana na serikali katika kufanikisha ujenzi wa miradi hiyo ya maendeleo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema wakati serikali ikijikita kwenye miradi ya ujenzi kama majengo ya kisasa, barabara, miundombinu ya maji, umeme na mengineyo, bila shaka itahitaji wataalam waliobobea, hivyo kwa upande wao wasiache fursa hizo.
Mhe. Hemed alifahamisha kuwa katika ujezi wa miradi hiyo ya maendeleo serikali imetoa nafasi ya upendeleo kwa wakandarasi wazawa ili waweze kutumia elimu na ujuzi walionao katika ujenzi wa nchi yao.
Amesema serikali itaendele kuwajengea uwezo wataalamu wazawa waweze kujiajiri na kuwajengea imani wawekezaji wanaowekeza nchini waweze kuwatumia katika shughuli za ujenzi wa miradi.
Aidha, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, amewasihi wahandisi na wakandarasi wote kuhakikisha wanazingatia ujenzi wenye viwango, kanuni na taratibu zilizoekwa na mamlaka ili kuepusha majanga yanayoweza kujitokeza.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Dk. Khalid Salum Muhammed, alisema wizara hiyo itahakikisha inasimamia wakandarasi, wasanifu na wakadiriaji majengo ili waweze kufanya kazi za kwa umakini, ubora na kwa kuzingatia viwango hatua itakayowezesha miradi kudumu kwa muda mrefu.
Dk. Khalid amesema serikali imepiga hatua zaidi katika suala la ujenzi wa miundombinu mbali mbali ikiwemo barabara, hospitali, majengo ya ofisi na mengineyo ambayo baadhi yao imejengwa na wakandarasi wazawa.
Nae rais wa taasisi ya wasanifu, wahandisi na wakadiriaji majengo Qs. Abdul Samad Mattar, amesema taasisi hiyo inapata ushirikiano wa karibu na taasisi mbali mbali ndani na nje ya nchi, kwa lengo la kupata kazi kwa pamoja zenye ubora, viwango na tija kwa taifa.
Amesema kufanyika kwa mkutano huo kumetoa fursa kwa viongozi na wanachama wa taasisi hio kujadili na kubadilisha utaalamu, ujuzi na uzoefu katika kuhakikisha wanaendelea kufanya kazi kwa ubora na uweledi wa hali ya juu.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mdhamini Mkuu wa Mkutano huo Shirika la Bima Zanzibar (ZIC), Hamida Juma alisema wameamua kudhamini mkutano huo ili kuendelea kujenga uhusiano mwema na wadau wao kwa kuendela kutoa huduma bora na za haraka zenye kuzingatia mahitaji ya wateja wao.
Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
Tarehe 14 - 06 - 2025
No comments:
Post a Comment