Habari za Punde

WAANDAAJI WA BAJETI WATAKIWA KUZINGATIA VIPAUMBELE

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya, akiwataka Wataalam wanaoandaa na kusimamia Bajeti ya Serikali kuzingatia vipaumbele vya miradi, wakati akifungua Kikao Kazi kuhusu  Mfumo wa Uandaaji na Usimamizi wa Bajeti (CBMS) ulioboreshwa, katika ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma.

Na. Josephine Majura na Peter Haule, WF, Dodoma

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya, amewataka Wataalam wanaoandaa na kusimamia Bajeti ya Serikali kuweka vipaumbele katika utekelezaji wa miradi ili kuepuka kutekeleza miradi nje ya bajeti iliyopangwa.

Wito huo umetolewa jijini Dodoma wakati akifungua rasmi Kikao kazi cha Wataalam wanaoandaa na kusimamia Bajeti ya Serikali awamu ya pili kuhusu kutumia Mfumo ulioboreshwa wa Uandaaji na Usimamizi wa Bajeti (CBMS) katika kusimamia bajeti na kushauri namna bora ya kutekeleza bajeti zao.

Bw. Mwandumbya alisema kuwa kuna baadhi ya maeneo ambayo wanaomba fedha za kutekeleza miradi nje ya bajeti mwezi mmoja baada ya bajeti kupitishwa jambo ambalo linatia mashaka katika upangaji wa vipaumbele vya utekelezaji wa bajeti.

Katika hatua nyingine aliwataka wataalamu hao kuangalia uwezekano wa kutekeleza miradi inayofanana kwa kushirikiana ili kuepuka kutumia rasilimali nyingi katika eneo moja ili kuleta tija.

“Yawezekana Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi zikawa na mradi wa umwagiliaji ambao utakidhi mahitaji ya mifugo na umwagiliaji lakini utakuta kila mmoja ana mradi wake, hili tunaliona ni changamoto kwa kuwa rasilimali ni zilezile, badala ya kuunganisha kuwa na mradi mmoja hata kama rasilimali itaongezeka kidogo kutakuwa na tija kuliko kila mmoja kutekeleza mradi wake”, alieleza Bw. Mwandumbya.

Aidha, alisema kuwa mwaka 2026/2027 utakuwa mwaka wenye bajeti inayotokana na vikaokazi vinavyoendeleza na utakuwa mwaka wa kwanza katika utekelezaji Dira ya Taifa ya 2050, hivyo ni vema kuangalia Dira inasemaje ili kuweza kupanga vizuri Bajeti kulingana na Dira hiyo.

Alisema kuwa katika kupanga bajeti ni lazima kuzingatia Dira ya Taifa lakini pia Ilani ya Chama ili kuwa na miradi ambayo inazingatia uelekeo wa nchi katika kipindi cha muda mfupi, wakati na mrefu ili kurahisisha upimaji.

Kikao kazi cha wataalam wa Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali na Sekretarieti za Mikoa kinatarajia kumalizika Agosti 29, 2025 kikijadili pia kuhusu mafanikio na changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2024/25, uandaaji wa bajeti ya 2025/26 na kupata maoni ya maandalizi ya  Mwongozo wa uandaaji wa  Mpango na Bajeti ya Serikali wa mwaka 2026/27.  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.