Katibu Mkuu Wizara ya Habari Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar Fatma Hamad Rajab ameahidi kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Ukuta (SQUASH) Afrika ili kuleta maendeleo ya Michezo hususan Mchezo huo.
Ameyasema hayo wakati Rais wa Shirikisho la Mpira wa Ukuta Afrika (SQUASH) Dr. Lucky Mlilo alipomtembelea huko Ofisini kwake Migombani Wilaya ya Mjini.
Aidha Katibu Fatma, amepokea kwa mikono miwili ombi la Raisi huyo, kuandaa mashindano Squash kwa Watu wenye umri wa miaka 35-85 (Masters) ambayo hayajawahi kufanyika Nchi yoyote Barani Afrika na mara ya kwanza, yanatarajiwa kufanyika Visiwani Zanzibar.
Hata hivyo amesema katika viwanja vitakavyojengwa katika Mji wa Michezo Fumba, wizara itahakikisha inajumuisha Viwanja vya Mpira wa Ukuta (Squash).
Kwa upande wake Kamishna Idara ya Michezo wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Ameir Mohammed Makame amesema, mashindano hayo, yataweza kutoa fursa kwa Wachezaji, kuongeza Mapato kwa Serikali na Wageni kutembelea sehemu mbalimbali.
Nae Rais wa Shirikisho la Mpira wa Ukuta Afrika (SQUASH)Dk. Lucky Mlilo amesema lengo la kuja Tanzania ni kutoa mafunzo kwa Wachezaji na Waamuzi wa Mchezo huo ambayo Tanzania bara yamefanyika wiki iliopita na upande wa Zanzibar yamefanyika leo.
Hata hivyo Rais huyo, ameiomba Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuboresha na kuweka mikakati inayokubalika kitaifa, kikanda na kimataifa ili kupata fursa ya kuandaa mashindano mbalimbali ya Mpira huo.
Ziara ya Rais wa Mpira wa Squash amefanya ziara Nchini kuangalia Changamoto wanazokabiliana nazo ili kuweza kuandaa mashindano ya kimataifa ambayo yanatarajiwa kufanyika Zanzibar hapo mwakani.
Imetolewa na kitengo cha Habari, WHVUM.
No comments:
Post a Comment