Na.Mwandishi Wizara ya Afya Zanzibar.
WIZARA ya Afya imesema Zanzibar imefanikiwa kusimamia utekelezaji wa sera ya Taifa ya dawa na kuhakikisha kuwa upatikanaji wa dawa muhimu na vifaa tiba pamoja kusimamia matumizi sahihi ya dawa.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Wafamasia Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya mnara wa kumbukumbu Kisonge Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dkt Mngereza Mzee Miraji amesema katika kipindi cha miaka mitano kumekuwa na mafanikio makubwa kupitia juhudi za wafamasia.
Aidha amefahamisha kuongezeka kwa upatikanaji wa dawa muhimu katika hospitali kutoka asilimia 57 hadi 95 na vituo vya Afya kutoka asilimia 63 hadi 96 na kufanikisha wananchi wanapofika kupata huduma hawapati usumbufu wowote katika sula zima la dawa.
Amesema mafanikio mengine yaliyopatikana katika sekta ya dawa ni kuimarika kwa bajeti ya dawa na vifaa tiba kutoka asilimia 51 hadi kufikia asilimia 98 sambamba na kuongezeka kwa idadi ya watumishi wa kada ya wafamasia kutoka 271 hadi 484.
Dkt Mngereza amewataka wafamasia kuhakikisha kila mwananchi anapata tiba sahihi, salama na yenye ubora na kuzingatia mabadiliko ya ulimwengu yanayobadilika kwa kasi huku changamoto za kiafya zikiongezeka kutokana na magonjwa sugu ya matumizi ya dawa yasio sahihi.
Sambamba na hilo amewaasa kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya taaluma waliyonayo na kufanya kazi kwa ushirikinao na kada nyengine za afya kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba.
Kwa upande wake Mfamasia Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Hidaya Juma Hamad ameipongeza taasisi inayosimamia usalama na ubora wa dawa pamoja wa kuwashukuru wafamasia wote wanaochangia kupeleka huduma ya dawa kwa jamii.
Aidha amesema katika kuimarisha huduma ya dawa ni vyema kuwe na mshikamano wa hali ya juu kwa wataalamu wote katika kulinda afya za wananchi kwa kuwapatia matibabu sahihi ili kuondokana na matatizo yanayosababishwa na dawa.
Nae Mwenyekiti wa Jumuiya wa wafamasia Zanzibar Ame Omar Ame amesema lengo la jumuiya yao ni kuwaunganisha wafamasia wote hapa nchini kwa madhumuni ya kuinua taaluma ya wafamasia na kuleta maslahi mapana juu ya fani hiyo.
Amefahamisha kuwa bila ya kufanya kazi kwa bidi taaluma ya wafamasia haiwezi kuonekana ambapo jamii inaendelea kunufaika na kazi zinazofanywa na wa wafamasia katika maeneo mbali ya sekta ya Afya.
Siku ya wafamasia duniani huazimishwa kila mwaka tarehe 25 ya mwezi wa tisa na ujumbe wa mwaka huu ni Fikiria Afya, Mfikirie mfamasia.
Mwisho
No comments:
Post a Comment