Habari za Punde

Wafanyabiashara wa Oman Watembelea Mkoa wa Pwani Kujionea Shughuli za Viwanda na Biashara

Ujumbe wa wafanyabiashara kutoka Oman umetembelea Mkoa wa Pwani kwa lengo la kujionea shughuli za viwanda na biashara, na kuangazia fursa za uwekezaji kati ya Tanzania na Oman katika sekta mbalimbali.

Ujumbe huo umeongozwa na  Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara na Viwanda Mkoa wa Al Wusta na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Chama cha Biashara na Viwanda cha Oman Dkt. Salem Al-Junaibi (Mb). 

Wakiwa mkoani humo, walitembelea Kiwanda cha Nyama cha Union Meat kilichopo Kibaha, ambapo walishuhudia uzalishaji wa nyama na kujadili uwezekano wa ushirikiano katika sekta ya kilimo na ufugaji, hususan bidhaa za viwandani kama nyama.

Wafanyabiashara hao pia walitembelea Eneo la Viwanda la KAMAKA na kuona maendeleo ya miundombinu pamoja na jitihada za Serikali za kuvutia wawekezaji wa ndani na nje.

Kesho, tarehe 8 Septemba 2025, ujumbe huo utatembelea makao makuu ya TCCIA na kusaini Mkataba wa Ushirikiano kati ya TCCIA ya Tanzania na Oman, na baadaye kushirki katika Mkutano wa Biashara na Uwekezaji utakaofanyika katika Hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam, ukiwahusisha washiriki kutoka sekta ya umma na binafsi.








No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.