Habari za Punde

Jeshi la Polisi Songwe Lakabidhiwa Gari Mbili za Kisasa Kuimarisha Ulinzi na Usalama

SACP Senga  akimkabidhi funguo za Gari  SSP Kadogosa kwa ajili ya matumizi ya Jeshi la Polisi Songwe. 

Kamanda Senga akiwa katika picha ya pamoja na SSP Kadogosa na Wakuu mbalimbali wa Jeshi la Polisi baada ya kumalizika kwa hafla ya kukabidhi gari kwa ajili ya Jeshi la Polisi Songwe.

Na Issa Mwadangala.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Augustino Senga, amekabidhi magari mawili mapya aina ya Robur Armored TLC300 kwa Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Mkoa wa Songwe kutoka kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Camillus Wambura.

Makabidhianao hayo yamefanyika Oktoba 23, 2025, katika ofisi ya Kamanda Mkoa wa Songwe iliyopo Vwawa Wilaya ya Mbozi Mkoani humo na mara baada ya kukabidhi magari hayo, SACP Senga alitoa shukrani za dhati kwa IGP Camillus Wambura na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuimarisha uwezo wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe kupitia upatikanaji wa vitendea kazi vya kisasa, huku akisema kuwa magari hayo yataongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku hususan katika kudhibiti ghasia, kulinda raia na mali zao, pamoja na kuimarisha amani na utulivu Mkoani humo.

Aidha, Kamanda Senga amesisitiza dhamira ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe kuhakikisha magari hayo yanatumika ipasavyo na yatatunzwa kwa uangalifu mkubwa ili yaweze kutumika kwa muda mrefu na Mkoa wa Songwe kuendelea kuwa salama.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoa wa Songwe, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Sija Kadogosa, ameahidi kutekeleza kwa vitendo maelekezo yote yaliyotolewa kuhusu matumizi ya magari hayo ili yawe chachu ya kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.