Habari za Punde

 

Mgombea Uwakilishi jimbo la Kiwani Ndugu Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na wanamichezo mbali mbali waliomo katika Jimbo la Kiwani na kutumia fursa hio kuwaomba kura ili aweze kuwa mwakilishi wa Jimbo hilo ifikapo Oktoba 29.

Mgombea wa Uwakilishi Jimbo la Kiwani ndugu Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali ya Awamu ya nane Imeboresha sekta ya michezo kwa kujenga viwanja vipya katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar na kufanya ukarabati mkubwa wa Uwanja wa New Aman Complex na Uwanja wa Gombani Pemba kwa lengo la kukuza sekta ya Mizo nchini.

Ameyasema hayo alipokutana na kuzungumza na wanamichezo mbali mbali waliomo katika Jimbo la Kiwani na kutumia fursa hio kuwaomba kura ili aweze kuwa mwakilishi wa Jimbo hilo ifikapo Oktoba 29.

Ndugu Hemed amesema anatambua changamoto mbali mbali zinazowakabili wanamichezo wa Jimbo la kiwani hivyo atakapokuwa mwakilishi wa Jimbo hilo  atahakikisha anaimarisha na kufufua vuguvugu la michezo jimboni humo.

Mgombea huyo amesema kwa sasa michezo ni ajira hivyo amewaahidi wanamichezo hao  kuwapa kila aina ya ushirikiano katika kufikia malengo yao ikiwemo kuwapatia vifaa vya michezo na mahitaji mengine yote yakimichezo.

Amesema kwa kutambua mchango na umuhimu wa michezo Jimboni na Taifa kwa ujumla atahakikisha analeta walimu na wakufunzi wa michezo mbali mbali watakao wafundisha kitaalamu ili kuwa na waamuzi, wachezaji, na timu bora zitakazoweza kushindana na timu yoyote ndani na nje ya Zanzibar.

Amewasisitiza wanamichezo hao kudumisha nidhamu kwa kufuata miiko, maadili na kanuni za michezo mbali mbali jambo litakalowajenga kuwa wanamichezo bora, pamoja na kuwataka kuwa na umoja, upendo na mshikamano baina yao.

Amesema katika kipindi cha uongozi wao wataunda kamati itakayohusisha timu zote zilizomo ndani ya Jimbo la Kiwani ambao watawasilisha kero na changamoto zinazozikabili timu zao kwa lengo la kulifanya jimbo la kiwani kuwa Jimbo la mfano kwa majimbo yote yaliyomo ndani ya Wilaya ya Mkoani na Zanzibar kwa ujumla.

Amewatoa hofu wanamichezo hao juu ya  suala la miundombinu ya Viwanja vya kufanyia Mazoezi na mashindano mbali mbali kwa kuwaahidi kuwa kushirikiana na viongozi wa michezo Jimboni humo atalisimamia suala hilo na kulipatia ufumbuzi.

Wakizungumza kwa niaba ya wanamichezo wenzao ndugu Yussuf Mohd Khatib na Ndugu Kassim Rashid Mohd wamesema wamekuwa wanakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo vifaa vya michezo, changamoto ya usafiri wanapokuwa na mashindano mbali mbali pamoja na uhaba wa walimu na wakufunzi wa kuwafundisha katika timu zao.

Wamesema viwanja vyao vya kufanyia mazoezi vimeathiriwa na ujenzi wa miundombinu ya barabara lakini pia wakati wa msimu wa mvuaa baadhi ya viwanja hujaa maji na kupelekea changamoto ya kukaa muda mrefu bila ya kufanya mazoezi jambo linaloathiri viwango vyao vya michezo.

Wanamichezo hao wamemuahidi Mgombea wa uwakilishi na wagombea wote wa chama cha mapinduzi kiwa watawachagua kwa kura nyingi za ndio ifikapo Oktoba 29 ili waweze kuwafanyia maendeleo makubwa zaidi jimboni mwao.

Imetolewa na kitengo cha Habari ( OMPR )

Leo tarehe 12 / 10 / 2025

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.