Imeletwa na Mdau kutoka ughaibuni
Hivi karibuni nilibahatika kutembelea visiwa vya Zanzibar nikiwa katika siku za mapumziko. Kwanza sina budi kutanguliza shukurani za dhati kwa Waislamu na wanaharakati kwa kuona maendeleo yanayoridhisha katika suala zima la Da’awah. Kwani madarsa yapo kwa wingi, Mihaadhara nayo pia hufanyika, makongamano ya kiislamu pia huandaliwa ikiwa ni juhudi za kuuendeleza Uislamu katika visiwa hivyi.
Pia kuwepo kwa taasisi za kiislamu ambazo zimeweza kutambua nini majukumu yake na kuyatekeleza ipasavyo katika kuielemisha jamii na kuitahadharisha katika yale ambayo ni wajibu kwa Waislamu kutahadharishana.
Mafanikio haya inawezekana si rahisi kwa mkaazi kuweza kuyaona lakini kwa mtu aliye mbali na kila akiji huona hali fulani ya mabadiliko ni jambo la kuridhisha sana.
Ila jambo moja lililonishitua ni kuona baadhi ya Wahaadhiri au Waalimu wanaosomesha katika madarsa mbali mbali na kuweza kutoa Mihaadhara kuweza kunasibishwa na darja ya kuwa ni Maulamaa.
Kuwa Aalim na kuwa ni Mwalimu ni vitu viwili tofauti. Mwalimu ni yule anaefundisha na kuelimisha iwe katika madarsa au hata maskuli na sehemu nyenginezo. Ama Aalim ni mwanazuoni aliebobea katika fani yake katika majala ya dini kwa kuweza kuifafanua na kuielezea, kuifanyia tafiti = buhuuth za kielimu na kubwa mpaka kunasibishwa kuwa ni Aalim ni kuweza kuwa na maandiko ya vitabu na tafiti ambavyo ameweza kuandika katika kufafanua moja katika maalumaati aliyojaaliwa. Tafiti hizi huwekwa kwenye majournals katika Vyuo Vikuu na huwawia rahisi wenye kufanya tafiti za kielimu kuweza kunufaika na matunda ya tafiti hizi.
Kitu ambacho ninaweza kudiriki kusema kwa uoni wangu wa karibu (mnaweza kunisahihisha nikikosea) ni kwamba suala la uandishi kwa wanaharakati za kidaawah ni dogo na finyu mno tena hasa kwa wale wanaotegemewa kuwa ni wanazuoni wetu.
Inawezekana kuwa ni mojawapo ya sababu ambapo wengi miongoni mwa wanaharakati hawajaelewa umuhimu wa kuandika katika dini. Madhara yake elimu aliyokuwa nayo pindipo akiondoka duniani hupotea isipokuwa chache iliyopokewa na wanafunzi wake. Lau kama ingeliandikwa basi faida yake ingewafikia wengi miongoni mwa Waislamu.
Pia inawezekana wengi hushindwa kuandika kwani baada ya kuandika kazi zao hushindwa kuendelea kufikia kuchapishwa kutokana na ughali wa gharama. Hivyo huona vigumu kujiingiza katika kazi ambayo hatima yake haieleweki. Ingawa nukta hii ina mantiki lakini katika ulimwengu wetu wa leo ambao kazi kama hizi zingeweza kunufaisha Waislamu zingeweza kupelekwa katika Tovuti za kiislamu kwa kuanzia ambako zingeweza kuleta changamoto katika kuhojiwa au kutolewa maelezo ya ufafanuzi hasa kwa wanaotembelea tovuti hizi ambazo licha ya jitihada za kuasisiwa bado zinakosa wachangiaji ambao tunaamini wanao uwezo wa kuandika mengi yanayohusiana na dini yetu.
Tuchukulie mfano mdogo wa Aalim na mwanazuoni anaeyeheshimika katika dini yetu. Imaam Annawawiy.
Imaam Muhiyyi Ddiyn Abu Zakariya Yahya bin Sharaf an-Nawawiy alifariki akiwa na miaka 45 . Lakini kazi zake alizoziacha katika maandiko ni za kupigiwa mfano kiasi cha kwamba nyingi ndizo zinazotegemewa katika mitaala ya ufundishwaji katika taasisi za kielimu nyingi ulimwenguni. Kwa wasiomjua ni mwandishi wa vitabu vingi kama kitabu cha hadithi arubaini za Nawawiy na Riyaadhu Swalihiin.
Kazi zake hazikutumiwa kama ni bahati tu bali ni kwa sababu ya mfumo wake wa uandishi na uhakiki mpaka zimeweza kukubalika na kuheshimika na miaka takriban mia nane tokea kufariki kwake bado anaendeleza sadaqatun jaariya hadi hii leo.
Tukija nyumbani na tumuangalie Sheikh Abdullah Swaleh Al Farsy Allah Subhaanahu Wata’ala amrehemu. Sheikh Abdullah aliheshimika enzi za uhai wake na anazidi kuheshimika hata baada ya kufariki na si kwa kumbukwa kwa elimu yake tu bali anaenziwa pia na kazi zake za kiuandishi ambazo wengi waliokuwa hawamfahamu vizuri wameweza kumjua vizuri Sh Abdullah kupitia vitabu vyake vyingi alivyoviandika na Tafsiri yake ya Qur-aan katika lugha ya Kiswahili. Sh Abdullah Swaleh alikuwa ni mtetezi wa Sunnah katika enzi zake lakini wengi hawakuweza kumuelewa au walimuelewa lakini walikuwa katika hali ya kugubikwa na hali za jamii zilizokuwepo. Tunaozisikiliza kanda zake za mawaidha katika siku hizi tunafaidika vyema na mafundisho ambayo wengi walidai kama ni mageni lakini Sh Abdullah tayari aliweza kuyatanabahisa miaka mingi iliyopita.
Hii ni mifano michache itakayoweza kukupa taswira ya hadhi ya uanazuoni ambayo inaakisiwa zaidi na uandishi ikia ni kama kumbukumbu ya kazi zilizofanyiwa kazi na kupitiwa kuhakikiwa na kisha kuchapishwa na kubaki kama Sadaqatun Jaariyah.
Kigezo cha kuwa ‘Aalim si daraja ndogo ni daraja ya juu katika mizani ya kielimu na hapa nitamtoa mfano mdogo wa Mtafiti mmoja wa mambo ya kidini kutoka nje ya nchi alipofika Zanzibar jambo la kwanza alilotaka ni apelekwe kwenye Duka la Vitabu vya kiislamu. Hakutaka kupelekwa kwenye vyuo Vikuu au kwenye taasisi za kiislamu bali alichotaka kuona ni vipi Waislamu wa visiwa hivyi walivyojizatiti katika suala la Uandishi. Kilichomsikitisha hakuona kazi zozote za maana ambazo zinaweza kuitwa kazi za kitaaluma katika vitabu vichache vilivyoandikwa katika lugha ya Kiswahili.
Hili tu linaweza kukupa taswira halisi ya suala zima la uandishi miongoni mwa Mashekhe na Wanaharakati za kid’aawah.
Nakumbuka mwaka 2008, nilipokuwepo Zanzibar, nilibahatika kukutana na mwanaharakati mmoja ambae alinisimulia kisa cha Kijana mmoja wa kijerumani aliyekuwa akifanya Shahada ya uzamili (Master’s degree) katika athari za da’awah katika Visiwa vya Zanzibar. Hii ndio ilikuwa Mada yake aliyoifanyia utafiti kupelekea kupata Shahada hii. Kwa mujibu wa mwanaharakati, kijana huyu alikuwa akitafuta watu muhimu wanaotegemewa katika suala zima la Da’awah ili aweze kuwahoji katika kukusanya data muhimu alizozihitajia kukamilisha utafiti wake.
Hata hivyo watu aliokuwa akitakiwa kuwasiliana nao ili kupata data na vielelezo vyenye kukubalika ilikuwa vigumu kwa kukosekana watu wenye sifa na vigezo kwa mujibu wa utafiti wake jinsi alivyoupanga. Badala yake aliwasiliana na watu ambao kwa mtazamo wa kijuu juu kuonekana ndio wenye sifa za kuweza kuelezea hali halisi ya Da’awah bila ya hata na kuwa na vielelezo vinavyokubalika kitaaluma. Ila walitegemea uzoefu wao katika kujihusisha kwao na harakati.
Suala linabaki Je tunao Maulamaa Zanzibar?. Ruhusa kuchangia
shk mtoa mada uislamu elimu yake haizingatii dgree au shahada za vyu vikuu wala kuandika vitabu vingi. jiulize mtume kaandika vitabu vingapi? maswahaba waliandika vitabu vingapi? tuanze na makhalifa na baadae maswahaba wengineo. kufundisha elimu misikitini aU KATIKA MARASA INATOSHA KUWA NI KUFIKISHA UJUMBE. MWENYE KUTAKA KUSSIKIA ATASIKIA NA ASIETAKA ATAZIBA MASIKIO.
ReplyDeleteMaudhui ya mada yenyewe imelenga katika sehemu maalum nayo ni Maulamaa.
ReplyDeleteNinakubaliana na wewe kwamba Mtume (SAW) hakuandika wala masahaba ila ufahamu wangu wakati wao hili halikuwa miongoni mwa kazi zao.Yaliyokuwa majukumu yao walityatekeleza kikamilifu kama kusimamisha dini, kujenga dola la kiislamu na kadhalika
Kufundisha kama ni katika madarsa au miskitini ni sehemu ya kufikisha ujumbe na suala linabaki pale pale huyu anaefikisha kwa kutumia njia hii tumhesabu kama na Aalim - msomi au mwanazuoni?
Si mliwatimua na wengine wamedhulumiwa nafsi zao sasa nini tena kuna ulamaa gani zanzibar? itabaki historia tu!!
ReplyDeleteah! alikuwapo fulani!
Nikichangia kwa anonymous ambae ameleta hoja nzuri kwamba Maulamaa wametimuliwa na klichobaki n historia.
ReplyDeleteHii implications zake ni kubwa sana kama tukitafakari kwani sijui tutaweza vipi kuwa na imani na masheikh wetu waliopo na vipi kizazi kijacho kitakavyoathirika kama hatujakuwa na hatua madhubuti za kuwaandaa