Habari za Punde

HOTUBA YA RAIS WA TANZANIA VIWANJA VYA LUMUMBA - DAR BAADA YA KUCHUKUWA FOMU YA URAIS WA TANZANIA

Kikwete: Serikali ya Kitaifa Zanzibar Sikuizua Mimi, Wala Rais Karume
Asema Jibu Liko Kwenye Mwafaka Kwanza 1999
Awasifu Wanzanzibari Kwa Kufanya Maamuzi ya Busara
Awatahadharisha WanaCCM Kutowadharau Wapinzani

Na Juma Khamis, Zanzibar Leo.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwe, amesema suala la kuundwa serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar halikuzuliwa na Rais Amani Abeid Karume wala yeye binafsi, kama watu wanavyodhani.

Alisema suala hilo lilikuwepo tokea zamani baada ya kufikiwa muafaka wa kwanza kati ya CCM na CUF mwaka 1999, ambao ulielezea uwezekano wa Zanzibar kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa, lakini inaonekana watu wamesahau.

Aliyasema hayo jana katika ofisi ndogo ya CCM Dar es Salaam, wakati akiwahutubia maelfu ya wafuasi wa chama hicho baada ya kuchukua fomu Tume ya Uchaguzi ya kuomba kuteuliwa kugombea Urais wa Tanzania katika uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba.
Aidha aliwakumbusha wana CCM kwamba utaratibu wa kuwa na serikali ya umoja wa kitaifa sio wa milele na kwamba katika mkutano wa Butiama walikubaliana kupitiwa kila baada ya miaka mitano.

"Mwafaka wa kwanza ulizungumzia uwezekano wa Zanzibar kuwa na serikali ya umoja wa kitaifa, hili sio jambo lililozuliwa na Rais Karume na Kikwete kama watu wanavyofikiria na kututungia majimba mabaya mabaya," alisema Kikwete.

Alisema kwa kufanya hivyo, Zanzibar haitakuwa nchi ya kwanza na kuzitaja nchi za Congo DRC, Zimbabwe, Kenya na Afrika Kusini kuwa na mfumo wa aina hiyo wa serikali ingawa baadhi yao zimeachana nao.

Amewashukuru Wazanzibari kwa kufanya maamuzi ya busara kwa kuchagua serikali ya umoja ingawa alikiri kwamba hayakuwa maamuzi rahisi.

"Kuna mazingira mengine lazima ushinde na wenzako, na mazingira haya ndio yaliyopo kwenye siasa za Zanzibar," alisema Dk. Kikwete.

Kikwete alisema mengi yametokea Zanzibar katika chaguzi zilizopita na kuitia doa jeusi Tanzania katika ulingo wa kimataifa, akitoa mfano wa mauaji ya watu 23 mwaka 2001, wakati yeye akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

"Dunia ilikuwa imetuchukia, dunia ilikuwa inatusikitikia, kuna wakati unakwenda wanakufokea na kukwambia watu gani nyinyi mnaoua watu, lakini mfumo huu mpya sasa utaleta Zanzibar bora iliyo na amani na kuheshimiana zaidi," alisema Rais Kikwete.

Kikwete ambae ni Mwenyekiti wa Taifa wa CCM aliwatahadharisha wanachama wa chama hicho kutovidharau vyama vya upinzani hata kama CCM inajiona kuwa na nguvu.

"Tufanye kampeni kama vile tunaweza kushindwa, acheni kabisa kusema hawatuwezi hata kidogo, kama hawatuwezi tuthibitishe kwa kura sio mdomo mtupu," alitahadharisha.

"Tuache kabisa kudharau, mdharau mwimba mguu huota tende na haiwezekani miguu yetu kuota matende," alisisitiza.

Kikwete aliwataka wanasiasa wa vyama vyengine kuendesha kampeni za kistaarabu kwa kujiepusha na lugha chafu za kukashifiana, kuandaa makundi ya wahuni kupiga watu mawe na kuvamia mikutano ya vyama vyengine, akisema kufanya hivyo ni sawa na uhuni.

Aliwambia wana CCM kuwa atarejesha fomu hiyo Agosti 19 kabla ya kampeni rasmi kuanza Agosti 21 ambazo zitadumu kwa siku 70 kabla ya siku ya uchaguzi.

Mapema mgombea mwenza Dk. Mohammed Gharib Bilal alisema chama cha CCM kimejengeka na yeye kupata fursa ya kuwa mgombea mwenza ni heshima kubwa kwake.

"Ugombea mwenza sio kitu nilichokiomba lakini kwa sababu nimetunukiwa nimeipokea kwa unyenyekevu mkubwa na niko tayari kufanya kazi na Rais Kikwete katika kuwatumikiwa wananchi," alisema Dk. Bilal.

Dk. Bilal aligombea nafasi ya Urais wa Zanzibar na kupewa nafasi kubwa ya kushinda, lakini CCM ilimpitisha kwa kura nyingi Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk. Ali Mohammed Shein, mwezi uliopita mjini Dodoma.

Awali Katibu Mkuu wa chama hicho, Yussuf Makamba akinukuu maandiko katika biblia alisema mtu wa kujisifu ni yule atokae vitani na sio anaekwenda vitani, akimaanisha kwamba Rais Kikwete ana mengi ya kujisifia na sio wapinzani.

Alisema mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya CHADEMA ,Dk. Wilbroad Slaa hana jipya kwa wananchi zaidi ya ajenda yake ya kukabiliana na ufisadi ambao hata Yesu aliuacha.

"Unaposema uongo usiumalize ili na kesho upate kusema, Dk. Slaa kashamaliza uongo wote na hana akiba yoyote ya kusema," alisema Makamba ambae pia alimkabidhi kadi ya CCM, Katibu wa CHADEMA wilaya ya Ilala baada ya kukihama chama hicho.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.