Habari za Punde

RAIS WA ZANZIBAR AKITOWA SALAMU ZA KUUKARIBISHA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHAAN KWA WANANCHI WA ZANZIBAR IKULU

r

RISALA YA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHaAN
YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA
BARAZA LA MAPINDUZI,
MHE. ALHAJ DK. AMANI ABEID KARUME,
AGOSTI, 2010 - RAMADHAN 1431

Bismillahi Rahmani Rahim

Ndugu Wananchi,
Assalaam Aleikum Warahmatullah Wabarakatuh
Ramadhani Karim

Namshukuru Mwenyezi Mungu, anayetukuzwa na kila kilichopo ardhini na mbinguni, Mola Karimu na Rahim, alietujaalia waja wake uhai tukaupokea Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, mwaka 1431 Hijriya au 2010 Miladiya. Ni wajibu wa kila mmoja wetu amshukuru kwa neema hiyo na tumuombe atujaalie uwezo na uzima ili tutekeleze kikamilifu maamrisho yote ya kumuabudu kama inavyotakiwa katika mwezi huu mtukufu.
Mwezi huu ni mwezi wa kufunga, yaani saumu kama alivyotuamrisha Mola wetu katika Kitabu chake Kitukufu, Quran, Surat AL-BAQARA, Aya 183:
"Enyi mlioamini, mmefaradhishiwa saumu, kama walivyofaradhishiwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mwenyezi Mungu."
Aya zinazofuatia za sura hiyo, mpaka ya 187, zinatufunza kutekeleza saumu na faida zake. Kwa mfano katika aya 184, tunaelezwa "....... Na mkifunga ni kheri kwenu, laiti mngelikuwa mnajuwa."
Pamoja na hayo, Mola wetu kwa rehma zake kwetu binadamu ametuteremshia katika mwezi huo kitabu kitukufu cha Qurani chenye kila aina ya mwongozo wa maisha bora duniani na kutuelekeza kwenye kheri za kudumu za peponi. Subhana Wataala anatuambia katika Aya ya 185:
"Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Quran kuwa ni uongofu na hoja zilizo wazi kwa watu ,,,,,"
Kutilia mkazo ubora wa saumu Mtume Muhammad S.A.W. alimuambia Sahaba mmoja ilipoingia Ramadhani:
"Ni juu yako kufunga kwani hakika saumu haina mfano wake (kwa malipo yake)."
Ndugu Wananchi,
Pamoja na kumshukuru Mola wetu kwa fadhila hiyo ya mwezi mtukufu wa Ramadhani inafaa tutafakari neema nyengine aliyotupa nchini kwetu. Hiyo ni amani na utulivu uliopo nchini kote ambao ninahakika utasaidia kuifanya Ramadhani ya mwaka huu hapa Zanzibar kuwa ya umoja kwa wananchi wake, upendo miongoni mwetu na kupenda kusameheana kwa njia mbali mbali.
Tukumbuke kauli ya Bwana Mtume iliyonukuliwa na Maimamu kadhaa kuwa: "Saumu ni kinga." Na tafsiri ni kuwa saumu ni ngao ya kujikinga na maovu yote, kwa mfano kudhulumu, kuiba, kutoa maneno machafu na yasiyofaa, kudanganya na kadhalika.
Ndugu Wananchi,
Kuhusu manufaa ya Ramadhani tunafundishwa kuwa mwezi huo umegawika sehemu tatu, yaani makumi matatu: kumi la Rehma, kumi la Kufutiwa Dhambi na kumi la Kinga na Moto wa Jahanamu. Huu ni mpango mzuri ambao tukiufuata tutajiona tunafanikiwa na mambo yetu ya kidunia na akhera na tunatekeleza ibada zetu kikamilifu.
Ni heshima kubwa ya Mola wetu Karimu kutuanzishia Ramadhani kwa kumi la Rehma, kwa sababu huo ndio ufunguo wa neema na kutuelekeza kustawisha yale tunayotaka na kuyapendelea nchini kwetu, na hakika yanahitajika duniani kote, nayo ni amani, utulivu na kutakiana mema. Hadith maarufu ya Bwana Mtume (SAW) inasema:
"Wanaorehemu wanarehemewa na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kurehemu. Warehemuni walio katika ardhi Atakurehemuni aliopo mbinguni."
Tutaona kwamba panapo moyo wa kurehemeana, kunajengeka imani nzuri, mahaba, upendo na umoja kwa jamii yote, na hapo kunakuwepo baraka, kheri na mafanikio kwa watu wote.
Ndugu Wananchi,
Nchi yetu imo katika mchakato mzima wa kujenga umoja, amani na utulivu wa kudumu ili tufanikiwe katika kujiletea maisha bora kwetu sisi, watoto wetu na vizazi vijavyo. Siku chache zilizopita tumefanya zoezi muhimu la kuwaachia wananchi kutoa uamuzi juu ya mustakabali wa nchi yao. Ni kwa bahati nzuri na ya kumshukuru Mola wetu, uamuzi wa walio wengi ulikuwa ni kukubali kufanyika mabadiliko ya mfumo wa Serikali yetu ya Mapinduzi na kuleta mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Ni matarajio yangu na ya wananchi kwa jumla kuwa sote sasa tutaelewa umuhimu wa mabadiliko hayo ambayo yatatuongoza katika misingi ya kudumisha amani na utulivu nchini. Ni muhimu tushirikiane tuyafanikishe.
Natoa wito katika mwezi huu mtukufu, wananchi sote tutafakari neema ya umoja na mshikamano na tutekeleze maamrisho ya Mola wetu aliotuambia katika Surat Al-Maidah – Aya ya pili:
"Na saidianeni katika wema na uchamungu, wala msisaidiane katika dhambi na uadui."
Tuchukulie rehma za mwezi mtukufu katika kujenga umoja na mshikamano wa watu wetu, kustawisha mapenzi baina yetu na kushikamana kwa kamba ya Mwenyezi Mungu, ili tuwe na utulivu na hali nzuri ya maisha. Tuelewe kwamba umoja wa wananchi ni miongoni mwa rehema za Mwenyezi Mungu kwetu.
Katika kuyathibitisha haya, Mwenyezi Mungu ametuamrisha katika Qurani Suratul Al-Imran aya ya 104:
"Na wawepo katika nyinyi watu wanaolingania kheri na wanaoamrisha mema na wakakataza maovu na hao ndio watakaotengenekewa."
Ndugu Wananchi,
Naomba pia tuitumie neema hii ya Ramadhani kujifunza na kufuata mema ya mwongozo wa Qurani. Ni bahati nzuri na ya kujivunia kwamba katika nchi yetu, wanachuoni na mashekhe wetu wanajitolea kuendesha darsa mbali mbali za Qurani, misikitini na majumbani kwa wanaume na wanawake. Katika mwezi huu, serikali imepunguza saa za kazi ili kuwapa nafasi watu kuishughulikia Ramadhani kwa ibada na mambo mengine ya kheri kama hayo ya kwenda kwenye darsa.
Kwa kuwa Qurani "uwongofu kwa watu", ni wajibu wetu kuhakikisha kwamba tunajenga misingi bora ya watoto wetu kwa kuwapa elimu ya dini yetu na kuwashajiisha na kuwahimiza kujifunza Qurani na tafsiri yake. Wazee na wengine ambao wanahudhuria darsa wanapaswa kutumia wanayojifunza kuelimisha watoto na wengine waliopo majumbani. Bwana Mtume (SAW) amesema:
"Aliye bora miongoni mwenu ni mwenye kujifunza Qurani na akaisomesha."
Ndugu Wananchi,
Katika kutafuta rehema za Mwenyezi Mungu, kama nilivyogusia, tunawajibu wa kushirikiana na kusaidiana katika kuifanya Ramadhani, nyepesi na yenye kutupa furaha. Katika mwezi huu wa saumu mahitaji ya vyakula na nguo yanakuwa mengi zaidi. Ni vyema wafanyabiashara, wachuuzi na wanunuzi wasidhulumiane, kwa bei, vipimo au ubora wa vyakula na vitu vyengine. Kila mmoja atafute nafuu ya kurehemeana na kwa msingi wa kushikamana na kupendana ili tufanikiwe kuwa na urahisi wa maisha katika mwezi huu mtukufu.
Wakati huo huo, nawaagiza maafisa wanaohusika na ubora na bei za bidhaa wajitahidi kutoa ushauri kwa wafanyabiashara juu ya kutenda haki na kuwachukulia hatua za kisheria wanaohatarisha maisha ya watu kwa kuwauzia bidhaa mbovu au zilizopitwa na wakati. Ni bahati nzuri kwamba usafiri wa bahari sasa umeimarika kutokana na kukamilika bandari ya Malindi, na kuziwezesha meli kubwa za bidhaa na mizigo kutoka nchi za nje kuitumia bandari hiyo kwa ufanisi zaidi na kuteremsha mizigo ikiwa katika hali nzuri. Natoa wito wa ushirikiano wa jamii yote katika jambo hili. Aidha, masheha na maafisa wa soko wahakikishe mazao yanayouzwa katika masoko yamepevuka. Tukumbuke kwamba Mwenyezi Mungu amekataza ufisadi wa mazao na ametaka yavunwe yanapokua tayari.
Wakati huo huo, ninafuraha kwamba hali ya upatikanaji maji na umeme katika nchi yetu imeimarika na ni ya kuridhisha. Kwa upande wa Pemba, umeme sasa ni wa kuaminika tokea tulipoanza kuupokea kwa njia ya bahari kutoka Tanga. Kwa Unguja tumefanikiwa kuweka majenereta ambayo yatakuwa tayari kutoa umeme wakati utakapokatika kutoka bara. Kwa upande wa maji, hali imeimarika ingawa bado huduma hiyo haijaweza kumfikia kila mwananchi. Naomba tuwe wastahamilivu wakati Mamlaka ya Maji imo mbioni kukamilisha awamu ya pili ya mradi mkubwa wa maji kwa Mkoa Mjini Magharibi na kuyapatia ufumbuzi matatizo yanayojitokeza sehemu nyengine. Kwa jumla, ni mategemeo yangu tutajitahidi kutumia maji na umeme kwa njia nzuri.
Ndugu Wananchi,
Kwa kumalizia, natoa tena shukurani kwa Mola wetu kwa neema na ukarimu wa kutupa uhai tukaipokea Ramadhani mwaka huu. Namuomba atujaalie kheri na ukarimu wake wa kuwa na Ramadhani nyingi zijazo - Amin.
Nasisitiza tena moyo wa kujenga na kustawisha umoja, mshikamano, amani na utulivu nchini. Tumuombe Mwenyezi Mungu ajaalie Leo yetu iwe ni bora kuliko Jana yetu; na ajaaliye Kesho yetu iwe bora kuliko Leo yetu.
Mwenyezi Mungu atuimarishie moyo wa imani, mahaba, upendo, umoja na mshikamano wa wananchi wote ili amani na utulivu vistawi na kutuletea mafanikio katika maendeleo ya nchi yetu.
Mola wetu tupe uzima na afya tutekeleze ibada ya Ramadhani na utujaalie saumu ya kukuridhisha na kutukubalia dua na funga zetu na utupe matarajio yetu ya kheri.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
RAMADHAN KARIM
KULLU AAM WA AANTUM BIKHEIR
WASSALAAM ALEIKUM WARAHMATULLAH WABARAKATUH

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.