Habari za Punde

WAANDISHI MNA MAJUKUMU YA KUFANIKISHA UCHAGUZI.

'Waandishi bado mna majukumu makubwa kufanikisha uchaguzi'

Na Halima Abdalla

MKURUGENZI wa Televisheni Zanzibar, Chande Omar amesema bado waandishi wa bahari wana majukumu makubwa katika kufanikisha chaguzi nchini kwa vile kazi yao ni muhimu katika wakati wote na zaidi kipindi cha Uchaguzi Mkuu.

Chande aliyasema hayo jana alipokuwa akifungua mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusiana na kuripoti habari za uchaguzi yaliowashirikisha waandishi wa habari kutoka vyombo mbali mbali vya Zanzibar.

Alisema kuwa mafunzo hayo yamekuja muda muafaka kwa waandishi kwani yataweza kuwasaidia katika kukusanya habari katika kipindi cha uchaguzi.

Alisema waandishi wa habari wanakabiliwa na changamoto kubwa katika kipindi hiki cha Uchaguzi, hivyo kupatiwa mafunzo hayo kutasaidia kwa kiasi kikubwa katika kazi zao.
Sambamba na hayo, amekipongeza Kituo cha Deutche Velle kwa kuandaa mafunzo hayo yenye lengo la kuwasaidia waandishi wa habari wa Zanzibar.

Alisema wandishi wa habari ni watu muhimu na kwamba lazima kazi yao waifanye kwa kuzingatia maadili, mipaka na wawe wenye uwezo katika kuitumia vizuri kalamu yao.

Nae Meneja wa Mpango wa mafunzo hayo, Kanda ya Afrika, Charles Achaye Ddong, alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwaandaa waandishi wa habari Zanzibar kuweza kuripoti habari za Uchaguzi katika Kipindi cha Uchaguzi.

Aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kuwa makini wakati wa mafunzo hayo kwani yatawasaidia kwa kuwapa uwezo mkubwa zaidi wa kuandika habari kwa usahihi na umakini zaidi.

Mafunzo hayo ya siku tano yameandaliwa na Kituo cha Deutche Velle cha Ujerumani ikishirikiana na Television Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.