Habari za Punde

IRELAND YAPONGEZA HATUA ZA MAENDELEO YA ZANZIBAR.


Balozi aahidi uwekezaji, amani utulivu wamridhisha
Dk. Karume asema uchaguzi utakuwa huru na haki
Rajab Mkasaba

IRELAND imeahidi kuendeza ushirikiano wake na Zanzibar na kueleza kuwa hatua zilizofikiwa kiuchumi, kisiasa na kijamii hapa nchini ni za kuungwa mkono.

Balozi wa Ireland nchini Tanzania Lorcan Fullam alisema hayo jana alipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Amani Abeid Karume, Ikulu mjini Zanzibar.

Katika mazungumzo yake, Balozi huyo alimueleza Rais Karume kuwa Ireland itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo kwani juhudi kubwa zimefikiwa.

Alieleza kuwa mafanikio yaliofikiwa katika sekta za maendeleo yameonesha wazi na juhudi kubwa alizozifanya Rais Karume katika uongozi wake wa awamu ya sita.

Balozi Fullam alieleza kuwa Ireland inajivunia uhusiano na ushirikiano kati yake na Zanzibar na kuahidi kuuimarisha zaidi kwa manufaa ya pande zote mbili.

Aidha, Balozi Fullam alieleza kuwa hatua za maendeleo ya kisiasa yaliofikiwa Zanzibar kwa kujenga umoja na mshikamano kwa kufanya maridhiano hivi karibuni ni mafanikio makubwa ambayo yataleta manufaa kwa nchi na wananchi wake.

Akieleza katika suala zima la uimarishaji katika sekta ya uwekezaji Balozi Fulaam alieleza kuwa nchi yake ina makampuni mengi ambayo yanaweza kuvutiwa kuja kuekeza Zanzibar katika sekta mbali mbali.

Pamoja na hayo, Balozi Fullam alitoa pongezi zake kwa Rais Karume kwa hatua nzuri iliyofikiwa katika kuhakikisha wananchi wanavitambulisho vya ukaazi na vya kupigia kura ambayo ni vya kisasa vilivyotumia teknolojia kubwa.

Akieleza juu ya hatua zilizofikiwa katika kuimarisha miradi ya maendeleo, Balozi Fullam alisema kuwa mazingira na mikakati madhubuti iliyowekwa katika kuimarisha sekta ya utalii hapa Zanzibar ndio chachu ya mafanikio katika sekta hiyo na kuahidi kuitangaza Zanzibar kiutalii nchini mwake.

Katika mazungumzo hayo, Rais Karume alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar nayo inajivunia uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati yake na Ireland.

Rais Karume alisema kuwa Ireland imekuwa ni miongoni mwa washirika wa maendeleo ambao wamekuwa wakiiunga mkono Zanzibar.

Akieleza juu ya mafanikio ya kisiasa yaliofikiwa hapa Zanzibar, Rais Karume alisema kuwa suala la umoja na mshikamano ni muhimu katika nchi inayojitafutia maendeleo kwani bila ya mashirikiano maendeleo hayawezi kupatikana.

Alieleza kuwa siku zote maendeleo huletwa kwa mashirikiano pamoja na kuwepo kwa amani na utulivu ambayo Zanzibar inajivunia hivi sasa.

Katika mazungumzo hayo Rais Karume alimueleza Balozi huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikichukua juhudi za makusudi katika kuhakikisha uchaguzi wa mwaka huu unakuwa wa huru na haki.

Aidha, Rais Karume alieleza kuwa kutokana na hali hiyo ndio juhudi zikachukuliwa katika kuhakikisha kila mwananchi mwenye sifa za kuwa na kitambulisho cha ukaazi na kile cha kupigia kura.

Rais Karume alimueleza Balozi huyo kuwa sekta mbali mbali za maendeleo zimeweza kupata mafanikio hapa nchini kwa kuwepo mashirikiano ya pamoja kati ya wananchi wa serikali yao sanjari na kuungwa mkono na washirika wa maendeleo.

Alisema kuwa sekta ya utalii ni miongozi mwa sekta za maendeleo zilizopata mafanikio makubwa na kuufanya utalii wa Zanzibar kuwa kivutio kikubwa kwa wageni kutoka nchi mbali mbali duniani.

Sambamba na hayo, Rais Karume alimueleza Balozi huyo kuwa juhudi zaidi zinachukuliwa katika kuimarisha zaidi sekta za maendeleo na tayari zimeonesha kuzaa matunda zikiwemo sekta ya elimu, afya, mawasiliano, miundombinu ya barabara, kilimo, maji, umeme na nyenginezo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.