Na Khamis Mohammed
WAZIRI wa Kazi Mandeleo ya Vijana Wanawake na Watoto, Asha Abdallah Juma, amesema athari za UKIMWI kiuchumi, kijamii na hata kisiasa ni kubwa hivyo watu wanawajibika kupima kwa hiari ikiwa ni njia muhimu katika kupambana na maambukizo ya UKIMWI.
Hayo aliyaeleza kwenye taarifa yake wakati wa uzinduzi wa mradi wa 'Kijana Amka Pima Kwa Hiari VVU kwenye mkutano na waandishi wa habari huko Mwanakwereke jana.
Taarifa ya Waziri Asha ilisomwa na Kamishna wa Kazi Zanzibar, Idi Ramadham Mapuri.
Waziri Asha alisema, iwapo wanajamii watapima hali za afya zao na kupata ushauri nasaha wanaweza kuepuka maambukizi mapya iwapo hawajaambukizwa na kuzuia maambukizo kwa aliyeambukizwa.
Alisema, Wizara ya Kazi Maendeleo ya Vijana Wanawake na Watoto kwa kushirikiana na Clinton Health Access Initiative (CHAI), imeamua mradi huo wa kuhamasisha vijana vijana kupima VVU kwa hiari kwa Zanzibar uanzie Mkoa wa Mjini Magharibi ambao una kiwango kikubwa cha maambukizi ikilinganishwa na vijijini.
Alisema, maeneo ya mjini yana muingiliano wa watu mbalimbali kiasi kwamba vishawishi vya kupelekea matamanio ya ngono isiyo salama na kupata maambukizi ya maradhi ya zinaa na VVU yana ushawishi mkubwa.
Alifahamisha kuwa umuhimu wa mradi huu katika mkoa wa Mjini Magharibi ni kuwahamasisha vijana mbalimbali wenye umri wa miaka 15-24 ili kujitokeza kwa vwingi kupima VVU kwa hiari na kujiwekea utamaduni wa kufuatilia afya zao mara kwa mara.
Hivyo, Waziri Asha aliyashauri makundi mbalimbali kujitokeza kupima afya zao na kuacha woga ili kujitokeza kupima kwa hiari kwa faida yao na taifa kwa ujumla.
"Njia mbalimbali zitatumika kuwahamasisha vijana kujitokeza ikiwemo tamasha la michezo ya mpira wa miguu, zenji fleva n.k", alieleza Waziri katika taarifa yake.
Aidha Waziri huyo, alisema, Uzinduzi wa tamasha la vijana utafanyika kiwanja cha kisonge na kuendelea katika viwanja mbalimbali vya wazi kwa kila mwezi mara mbili kwa wilaya zote za Mkoa huo.
Kiasi cha shilingi milioni 860 zinatarajiwa kutumika katika mradi huo unaohusisha Mikoa minane ya Tanzania ambapo kwa Zanzibar ni Mkoa wa Mjini Magharibi.
No comments:
Post a Comment