Dk.Karume ampa meno Mdhibiti Mkuu Zanzibar
Asema ni kufanikisha utawala bora, maendeleo
Na Mwanajuma Abdi
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume amesema Serikali imetoa uhuru kwa Afisi ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa serikali kufanya kazi kukagua, kuhoji na kusimamia fedha bila kuingiliwa na Taasisi yoyote.
Alisema hatua hiyo ni moja ya hatua kadhaa zinazotekelezwa na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kufanikisha dhana ya utawala bora nchini.
Rais Karume alitoa tamko hilo jana, wakati akifungua jengo jipya la Afisi hiyo, lililoko mtaa wa Maisara mjini hapa, ambalo ujenzi wake umechukua miezi sita na kugharimu shilingi milioni 267, zilizotolewa na Serikali.
Alisema Afisi hiyo imepewa mamlaka ya kisheria na katiba kusimamia ufanisi wa kuhoji na kudhibiti fedha za mali ya Serikali kwa Taasisi na wizara, bila kuingiliwa katika kufikia malengo ya utawala bora kwa sababu fedha hizo ni za wananchi kutokana na michango mbali mbali ikiwemo kodi.
Dk.Karume amesema uhuru huo umesaidia kudhibiti mapato ya Serikali kuu, ambapo maendeleo yaliyofikiwa mjini na vijijini ya kusambazwa kwa barabara, maji, kupiga vita malaria zinatokana na fedha hizo ambazo zingaliachwa kiholela mafanikio hayo yasingepatikana.
Aidha alieleza kuwa washirika wa maendeleo wameridhika na matumizi ya misaada ya fedha wanazochangia kupitia miradi mbali mbali kwa kuzipitishia kwenye bajeti kuu ya Serikali.
Aliipongeza Wizara ya Fedha na Uchumi kwa kuanzisha mfumo mzuri wa matumizi ya mawasiliano ya teknolojia "IFMS' kuwasiliana na Taasisi za Serikali kwa kupanga mikakati bora ya utoaji mishahara, malipo ya wastaafu.
Nae Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Katiba na Utawala Bora, Ramadhan Abdallah Shaaban, amesema uhuru wa kufanya kazi bila kuingiliwa umewezesha kupatikana ufanisi mkubwa, ambapo hivi sasa mkakati zaidi umeelekezwa kwa Taasisi zote zinaponunua vifaa au kutengeneza, gharama watazotumia zilingane na thamani ya kitu chenyewe ili kudhibiti fedha na mali ya Serikali.
Mapema akizungumza kwenye hafla hiyo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Fatma Mohammed Said, aliishukuru Serikali kwa kutoa fedha zote za ujenzi wa jengo hilo.
Mdhibiti huyo alieleza Afisi hiyo ilijipangia mikakati katika miaka mitano kuanzia mwaka 2006 hadi 2011, kuimarisha mazingira mazuri ya kazi, kujenga Afisi za kisasa Unguja na Pemba, ambapo mwakani inatarajia kujengwa afisi nyengine Tibirinzi kisiwani Pemba.
Alisema kwa upande wa mafunzo wafanyakazi wa taasisi hiyo, yenye vifaa vya kisasa vya teknolojia, ambayo pia imezindua tovuti yake, imewapatia mafunzo ya muda mrefu na mfupi idadi kubwa ya wafanyakazi wake.
Aidha alifahamisha kuwa, serikali imefanikiwa kutayarisha stahiki na maslahi ya wafanyakazi kulingana na utaratibu uliopangwa kwa kuzingatia umuhimu wa shughuli za ukaguzi pamoja na taaluma za wafanyakazi, lakini hadi leo utekelezaji wa stahiki na maslahi hayo haujafanikiwa kutekelezwa.
Ujenzi wa ofisi hiyo umefanywa na kampuni ya kizalendo ya Stars Construction, pamoja na mitandao kuwekwa na vijana wa hapa nchini.
No comments:
Post a Comment