Habari za Punde

WANANCHI WAJITOKEZA KUPIGA KURA LEO

Na Issa Mohammed/Halima Abdalla/ Suleiman Almasi

WANANCHI wa majimbo ya Mji Mkongwe na Magogoni, Mkoa Mjini Magharibi watalazimika kurudia uchaguzi kwa nafasi za Ubunge na Udiwani baada ya karatasi za kupigia kura kwa nafasi hizo kuchamganyika.

Hitilafu hizo ni kuchanganyika picha za wagombea ubunge katika jimbo la Magogono na za wagombea udiwani katika wadi mbali mbali za jimbo Mji Mkongwe.

Msimamizi wa kituo cha kupigia kura cha Bwawani katika jimbo la Mji Mkongwe, Rehema Othman Salim na msimamizi wa kituo cha upigaji kura cha Mtoni kidatu Juma Khamis Makame wamethibitisha kujitokea kwa hitilafu hizo.

Wakizungumza na Zanzibar leo kwa nyakati tofauti, walisema uchaguzi wa kuwania nyadhifa hizo utafanyika katika tarehe itakayopangwa.

''Kumejitokeza hitilafu katika karatasi za kupigia kura kwa mfano waliyekuwa akiwania ubunge picha yake imewekwa katika nafasi ya Udiwani na aliyeomba Udiwani picha yake imewekwa kwenye nafasi ya Ubunge,'' walisema wakuu hao
Hata hivyo, kwa jumla hali ya upigaji kura katika majimbo mbali mbali ya Mkoa Mjini Magharibi imekwenda vizuri na hakukua na matukio ya uvunjifu wa amani.

Wananchi wengi walijitokeza mapema katika vituo vya kupigia kura wakiwa na shauku ya kuitumia haki yao ya kimsingi na kidemokrasia ya kupiga kura, licha ya mvua kubwa ilikuwa ikinyesha wakati wa asubuhi.

Kutokana na wapiga kura wengi kufika mapema kkwenye vituo vya kupigia kura, baadhi ya vituo hivyo hadi ilipofika majira ya saa saba mchana vilikuwa na wapiga kura wachache na vingine havina kabisa.

Miongoni mwa vituo hivyo ni Mtofaani na Regeza Mwendo katika jimbo la Dole, wilaya ya Magharibi Unguja ambapo wahudumu wake walilazimika kukaa wakisubiri mtu mmoja mmoja aliyechelewa kufika kituoni.

Polisi ambao waliwekwa katika vituo mbali mbali vya upigaji kura hawakuwa na kazi ngumu tofauti na uchaguzi uliopita kutokana na wapiga kura kufuata taratibu za uchaguzi.

Katibu Mkuu wa chama cha CUF ambae anawania kiti cha urais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, alipiga kura katika kituo cha upigaji kura cha Mtoni Kidatu, saa 4.30 asubuhi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.