Na Mwanajuma Abdi
JUMLA ya wanafunzi 25,133 wanatarajiwa kufanya mitihani ya Taifa ya kumaliza darasa la saba itayoanza Jumatatu ya Novemba 22 hadi 25 mwaka huu.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ramadhan Abdulla Shaaban, alitoa taarifa hizo jana, kwa vyombo vya habari huko Mazizini nje kidogo wa Mji wa Zanzibar, mara baada ya kukabidhiwa Ofisi hiyo na aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo, Haroun Ali Suleiman.
Alisema wanafunzi 21,465 wa kidato cha pili wanatarajiwa kufanya mitihani yao ya kitaifa wiki inayofuata ya Jumatatu Novemba 29 na kumalizika Disemba nne.
Alifafanua kuwa, watahiniwa 25,133 wa darasa la saba wataofanya mitihani hiyo wavulana ni 11,558 na wasichana watakuwa 13,575.
Alieleza kwa upande wa kidato cha pili watahiniwa wote ni 21,465 lakini kati ya hao wanaume ni 9,849 na wanawake ni 11,616, ambao ndio wanatarajiwa kufanya mitihani hiyo ya kumaliza darasa la 10 na kuweza kufaulu kuingia darasa la 11.
Waziri Shaaban alisema mitihani hiyo ndio kipimo cha kujua uwezo wa wanafunzi baada ya kumaliza elimu yake ya msingi na sekondari ya lazima ili aweze kuchaguliwa kuendelea na masomo yake.
"Mtihani wa darasa la saba hutoa fursa ya kuchagua wanafunzi waliofanya vizuri na kuchaguliwa kuingia katika madarasa ya mchepuo yaliyoko katika skuli mbali mbali za sekondari pamoja na mtihani wa kidato cha pili hutoa fursa ya kuchagua wanafunzi waliofanya vizuri kuendelea na masomo katika kidato cha tatu na nne", alisema.
Alifahamisha kwamba, kutokana na hali hiyo alitoa wito kwa wazazi na walezi wa watahiniwa kuwahimiza watoto wao kufuata kanuni na taratibu za mitihani zilizowekwa ikiwemo kufika mapema katika vituo, kuchukua vifaa vyote muhimu vinavyohitajika kufanyia mtihani kama kalamu, penseli, raba, boski la kampasi na gamba la kuwekea karatasi ambalo halijachorwa na wajisomee zaidi ili waweze kufaulu.
Aidha aliwaelekeza watahiniwa hao waache kuchukuwa vifaa visivyohitajika katika mitihani ikiwemo simu za mikononi, sambamba na kutokatoka nje ya chumba cha mitihani kabla ya kutimia nusu saa tokea kuanza kwa zoezi hilo na kutowasiliana na mtu yoyote ndani au nje ya chumba cha mtihani isipokuwa msimamizi.
Tahadhari nyengine zilizotolewa ni wananchi wasiohusika na shughuli za mitihani wasipite katika maeneo ya skuli wakati zoezi hilo likiendelea pamoja na wasimamizi wa mitihani wahakikishe wanatekeleza dhamana zao kwa haki na uadilifu mkubwa.
Hata hivyo, alisema hivi karibuni kumeibuka vitendo vya udanganyifu wa mitihani kwa baadhi ya wanafunzi, hivyo aliwaonya wasijiingize katika jambo hilo kwani hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yoyote ataebainika kufanya tendo hilo au atayemsaidia mwenzake.
Alieleza kwamba udanganyifu katika mitihani hauwasaidii wanafunzi na mara zote huathirika kutokana na vitendo hivyo, ambapo wanaobainika hufutiwa matokeo ya masomo yote hata kama undanganyifu umeonekana katika swali moja au katika somo moja.
Waziri Shaaban aliongeza kusema kwamba, katika mwaka 2006 kesi za udanganyifu zilikuwa 37, mwaka 2007 zilikuwa 108, mwaka 2008 kesi zilikuwa ni 64 na mwaka jana zilichuka hadi kufikia 22, ambapo wanafunzi hao walifutiwa matokeo yao.
No comments:
Post a Comment