Habari za Punde

WAZIRI MPYA WA ELIMU KUENDELEZA ALIPOACHIA HAROUN

Na Mwanajuma Abdi

WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ramadhan Abdulla Shaaban amesema maendeleo yamefikiwa Waziri mpya wa Elimu kuendeleza alipoachia Haroun katika sekta ya elimu na kusababisha kuongezeka idadi ya kufaulu wanafunzi kuingia sekondari hadi vyuo vikuu hapa Zanzibar.

Kauli hiyo alitoa jana, wakati alipokabidhiwa Wizara hiyo, na aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo, Haroun Ali Suleiman, huko Mazizini nje kidogo wa mji wa Zanzibar.

Alisema sekta hiyo imekuwa na mafanikio makubwa katika miaka 10 kwa kuongeza idadi ya wanafunzi kufaulu, ambapo wakati wa nyuma ilikuwa ajabu wanafunzi kufaulu lakini kwa sasa hali kila ikisogea mbele kila mwaka idadi inaongezeka.

Alieleza mbali ya maendeleo hayo pia suala la vitabu kwa wanafunzi sio tatizo kuanzia msingi hadi sekondari, ambapo alimshukuru aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo Haroun kwa jitihada zake kubwa za kufikiwa mafanikio hayo kwa kushirikiana na watendaji wake.

Aidha aliongeza kusema kwamba, mradi mkubwa wa ujenzi wa skuli za sekondari katika mashamba mbali mbali umekuwa chachu katika maendeleo ya kunyanyua elimu, ambapo aliwaomba watendajia wa Wizara hiyo kuendelea kumpa mashirikiano ili kuwasaidia vijana kuwajengea mustakabali mzuri wa maisha yao ya baadae kwani bila ya taaluma mambo yanaweza kuwa magumu kwao.

Aidha waziri huyo aliahidi kuendeleza yale yote ya kimaendeleo yaliyoachwa na waziri huyo aliyehamishiwa wizara nyengine.

Nae Haroun Ali Suleiman alisema katika kipindi cha miaka 10 ya chini ya uongozi wa Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume ametoa mchango mkubwa wa kusaidia maendeleo katika sekta hiyo nchini.

Alisema wanafunzi wa kidato cha nne walikuwa wanafaulu kwa asilimia 31 huko nyuma lakini kwa sasa imefikia zaidi ya asilimia 54, jambo ambalo limewezesha kufunguliwa kwa madarasa mengi ya kidato cha tano katika skuli mbali mbali za Unguja na Pemba.

Hata hivyo, alimueleza Waziri Shaaban kwamba ameiwacha Wizara hiyo ikiwa bado inakabiliwa na tatizo la uhaba wa walimu wa sayansi katika skuli za sekondari pamoja na vikalio vya skuli, hivyo alimshauri jitihada zaidi na nguvu zake aelekeze huko katika kuyatafutia ufumbuzi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.