KATIBU Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM Tanzania, Martin Shigela amemvisha ukamanda wa vijana wilaya ya mjini, Mussa Aboud Jumbe.
Sherehe hizo zilifanyika katika Tawi la CCM kilimani, ambapo Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Tauhida Galos Nyimbo alimvisha joho hilo la ukamanda kwa niaba ya Katibu mkuu, Shigela.
Mwenyekiti huyo, alisema Jumbe amekuwa akijitolea na yupo mstari wa mbele katika kutoa misaada mbali mbali kwa UVCCM, ambapo Taifa limeona ipo haja baada ya kumchunguza na kuamua kumkabidhi ukanda huo, ambao kutokana na uweledi na uwezo mkubwa alio nao hadi Mkoa wataweza kumtumia.
Alieleza uteuzi wake unastahili kulingana na harakati zake alizokuwa akizifanya bila ya kuchoka katika kukitumikia Chama hususani katika Umoja wa Vijana.
Aidha, aliwapongeza Vijana kwa kufanya kazi kubwa katika uchaguzi mkuu uliomalizika hivi karibuni kuanzia shehia, wadi hadi taifa, jambo ambalo limesaidia Dk. Ali Mohammed Shein kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kupatikana kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na wabunge, wawakilishi na madiwani wa chama hicho.
Nae Kamanda wa Vijana wa CCM Wilaya ya Mjini, Mussa Aboud Jumbe aliwashukuru viongozi wa jumuiya hiyo kwa kumpendekeza jina lake hadi leo akavalishwa joho hilo, ambapo aliahidi kuendelea kukitetea chama hicho na kuwapigania vijana katika masuala ya kimaendeleo.
Alifahamisha kuwa, CCM ni chama imara kama ilani yake ya uchaguzi ilivyokuwa ikisema kwamba Ushindi ni lazima, jambo ambalo limedhihirika kutokana kushinda kwa kishindo na kubakia katika madaraka Zanzibar na Tanzania mzima.
Jumbe ambae ni Mkurugenzi wa Uvuvi na Mazao ya Baharini, alisema kazi nzito imekamilishwa ya kukiweka chama katika madaraka na kinachobakia kwa sasa ni kushirikiana katika kuijenga nchi kimaendeleo katika kipindi cha miaka mitano.
Aidha aliwashajiisha vijana kuwasaidia viongozi waliowepo madarakani katika kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kimaendeleo ya haraka, kwani vijana wa sasa sio wale wa miaka 20 iliyopita hivi sasa maisha yanakwenda kwa kasi kubwa na maendeleo yawe yanakwenda sambamba.
No comments:
Post a Comment