Habari za Punde

TANZANIA IMEPATA MAENDELEO YA MILENIA - DK SHEIN

Na Rajab Mkasaba, Tripoli Libya

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa nchi za Afrika ikiwemo Tanzania, zimepata maendeleo makubwa katika kutimiza malengo ya Milenia.

Dk. Shein aliyasema hayo leo katika hotuba yake aliyoitoa kwenye Mkutano wa Mashirikiano ya Kimaendeleo kati ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya, Mkutano unaoendelea huko Tripoli, nchini Libya.

Katika maelezo yake. Dk. Shein alisema kuwa miongoni mwa maeneo ambayo Tanzania imepata mafanikio katika kutimiza malengo ya Milenia ni elimu ya amsingi, kupunguza vifo vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, kupambana na Malaria pamoja Ukimwi.

Akitoa maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa hatua hiyo ya maendeleo iliyofikiwa na Tanzania inatokana na mashirikiano makubwa iliyopata kutoka kwa Washirika wa Maendeleo ambao wameweza kuiunga mkono Tanzania ikiwemo Jumuiya ya Ulaya (EU).

Dk. Shein alichukua nafasi hiyo kwakutoa shukurani kwa Washirika hao wa Maendeleo kwa kuweza kuiunga mkono Tanzania na kueleza mataraji yake kuwa Washirika hao wataendelea zaidi.

Dk. Shein ambaye amemuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mkutano huo, alimpongeza Rais wa Afrika ya Kusini Mhe. Jacob Zuma kwa kuingiza mada ya kilimo na chakula, mada ambayo inaelimisha na kuweza kutoa muelekeo kwa Afrika.

Alisema kuwa licha ya mafanikio yaliopatikana pia, Tanzania inakabiliwa na changamoto mbali mbali ambazo zinahitajika kuchukuliwa hatua ili kufikia lengo lililokusudiwa.

Dk. Shein alisema kuwa kutokana na tafiti mbali mbali zilizofanywa na zinazoendelea kufafanywa zimeonesha kuwa Afrika haitoweza kutimiza Malengo yote ya Milenia yaliyowekwa na badala yake mashirikiano zaidi yanahitajika kwa pamoja.

Dk. Shein alisisitiza kuwa mkazo zaidi unahitajika kwa nchi za Afrika katika kuimarisha sekta ya afya, chakula, elimu jinsia pamoja na usimamizi mzuri juu ya watu wenye mahitaji maalum.

Alisema kuwa iwapo nchi za Afrika itazitumia vyema rasilimali zake na kuimarisha mashirikiano ya pamoja anamatumaini makubwa kuwa mafanikio yatapatikana na kuwawezesha watoto kuishi maisha bora pamoja na wanawake hasa wale wanaoishi vijijini.

'Watoto watakwenda skuli vizuri na wananchi wataishi vizuri katika nchi zao bila ya kujali tofauti zao kijinsia, umasikini utatokomwezwa'alieleza Dk. Shein.

Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa suala zima la kilimo na chakula ni jambo muhimu sana katika nchi za Afrika kwa kutambua kuwa Uchumi wa Afrika unategemea sana kilimo.

Kutokana na umuhimu huo, Dk. Shein alieleza kuwa Tanzania imekuwa ikifanya juhudi za makusudi za kuhakikisha sekta ya kilimo inapata mafanikio kwa kuweza kuweka mikakati mbali mbali.

Alisema kuwa Tanzania imeweza kutia saini Programu ya Maendeleo ya Kilimo kwa Afrika (CAADP) kwa kutambua umuhimu wake mkubwa katika maendeleo ya Taifa katika sekta ya kilimo.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa iwapo mafanikio zaidi yanahitajika kuna haja ya kuongezwa upatikanaji wa fedha na mashirikiano zaidi kutoka Mfuko wa Fedha wa Ulaya (EDF) na nyenginezo.

Kutokana na hatua hiyo, Dk. Shein alisisitiza kuimarisha na kuongeza zaidi mikakati ya mashirikiano kwa nchi za Afrika.Pia, alisisitiza haja ya kuendeleza mafanikio ya kisiasa kwa nchi za Afrika.

Aidha, Dk. Shein alisisitiza haja ya kuwepo kwa mashirikiano ya pamoja katika kufikia malengo kwa nchi za Afrika ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa soko la pamoja.

Dk. Shein alitoa pongezi kwa Kiongozi wa Libya Mhe. Muammar Gaddafi, kwa maandalizi mazuri ya mkutano huo wa tatu wa EU na AU ambao mkutano wa mwisho kama huo ulifanyika miaka mitatu iliyopita nchi Ureno

Mkutano huo unatarajiwa kumaliza leo ambapo mada mbali mbali zilizungumzwa na kutolewa michango na viongozi mbali mbali waliohudhuria katika mkutano huo ikiwemo suala zima la uhamiaji, nishati, kilimo, uchumi, uwekezaji,mazingira, ushiruikiano wa kikanda, Malengo ya Milenia na nyenginezo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.