Na Rajab Mkasaba Tripoli, Libya
MAKAMO wa Rais wa Kenya, Mhe. Kalonzo Musyoka amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza Mapinduzi Mhe. Ali Mohammed Shein kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Pongezi hizo amezitoa wakati alipokuwa na mazungumzo na Dk. Shein mjini Tripoli, Libya ambako viongozi hao wote walihudhuria katika Mkutano wa tatu wa Mashirikiano kati ya Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Ulaya.
Katika mazungumzo hayo, Mhe. Musyoka alitoa pongezi kwa Zanzibar kwa kuendesha uchaguzi wa amani na utulivu na kuweza kujijengea sifa kubwa ndani na nje ya nchi.Mhe. Musyoka alimueleza Dk. Shein kuwa Kenya itaendeleza uhusiano na ushirikiano na Zanzibar uliopo ambao ni wa muda mrefu.
Aidha, alisema kuwa ana matumaini makubwa kuwa Zanzibar itazidi kupata mafanikio makubwa chini ya uongozi wa Dk. Shein.
Nae Dk. Shein alitoa shukurani kwa Rais Mwai Kibaki kutokana na salamu za pongezi alizomtumia kwa kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa Zanzibar na kumueleza Mhe. Musyoka kumfikishia kiongozi huyo salamu za shukurani kutoka kwake. Aidha, Dk. Shein alimueleza Mhe. Musyoka kuwa Zanzibar inathamini uhusiano na ushrikiano uliopo kati yake na Kenya.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alisisitiza umuhimu wa kuendeleza mashirikiano yaliyopo kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ili ziweze kupata mafanikio makubwa zaidi.
No comments:
Post a Comment