Habari za Punde

TIMU ZA TOGO,IVORY COAST ZAALIKWA ZANZIBAR

TIMU za Taifa za Togo, Ivory Coast zimealikwa mjini Zanzibar kushiriki mashindano maalumu yatakayohusisha nchi nne. Akizungumza kwa simu jana kutoka Zanzibar, Katibu Mwenezi wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), Maulid Hamad Maulid alisema maandalizi kuhusiana na mashindano hayo yanaenda vizuri.

"Togo wao walituma maombi ya kuja Zanzibar kucheza mechi ya kirafiki na timu yetu ya Taifa, itakuwa walituona kwenye televisheni wakati wa michuano ya Chalenji.

"Lakini wakati hilo likifanyika, kuna mashindano ya nchi nne yanaandaliwa, ambayo tarehe rasmi itatangazwa hivi karibuni, yatafanyika hapa Zanzibar.

"Nchi hizo ni Ivory Coast, Togo, Zanzibar na Tanzania Bara ambayo timu yake ya Taifa Kilimanjaro Stars ilichukua ubingwa wa Chalenji Jumapili," alisema Maulid. Hata hivyo hakutaka kuingia kwa undani kuhusiana na suala hilo zaidi ya kusisitiza kuwa mambo ya maandalizi yanaenda vizuri.

Wakati huohuo, Maulid alisema kocha wao wa timu ya Taifa 'Zanzibar Heroes', Stuart Hall bado hajavunja mkataba nao hivyo akisaini timu yoyote kwa sasa bila kwanza kuvunja mkataba itakuwa ni kosa.

"Tunajua anafanya mazungumzo ya kuifundisha Azam lakini hajaleta barua ya kuvunja mkataba na sisi, kwani ana mkataba wa miaka mitano, hivyo akienda kinyume chake tutafikishana mbali," alisema Maulid.

Katika hatua nyingine, Maulid alisema kuwa Rais wa ZFA, Ali Ferej Tamim ametangaza kuwania tena nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Desemba 31, mwaka huu Gombani, Pemba. Maulid alisema ,Tamim alieleza nia yake jana mjini Zanzibar, ambapo leo fomu za wanaowania nafasi mbalimbali za uongozi wa ZFA zitaanza kutolewa

Chanzo: Habari Leo

1 comment:

  1. Sheikh Othman Tunashukuru sana kwa kutukumbusha sisi tulio mbali na nyumbani habari hizi nitawafikishia na wezangu Ishallah na m/mungu akujalia moyo waimani najua sio kazi ndogo hii yakukumbusha na kuka mda wote, kwa kutufikiria sisi tuliokuwa hatujui. M/mungu akujalie imani afya njeema pamoja na nguvu kwa hapari nyeti Ameen!

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.