Na Salum Vuai, Maelezo
TAKRIBAN wiki mbili baada ya kutolewa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF), uongozi wa klabu ya KMKM umemvua ukocha Juma Sheha na nafasi yake kukabidhiwa Ali Bushiri.
Sheha aliyeichukua timu hiyo kutoka kwa Abdulghani Msoma na kuinusuru kuteremka daraja na hatimaye kushika nafasi ya pili kwenye ligi kuu msimu uliopita, atakuwa nje ya shughuli zote za ufundishaji katika kikosi hicho.
Tayari Bushiri ameanza kazi ya kuinoa timu hiyo na kufuzu jaribio la kwanza kwa kuifunga Mundu katika mchezo wa ligi ndogo ya 'premier' kwa magoli 2-1 Machi 6, katika uwanja wa Mao Tsetung.
Katibu Mkuu wa wanamaji hao Sheha Mohammed, alisema kabla hajakabidhiwa mikoba hiyo, Bushiri alimuandikia Mkuu wa kambi kuomba kazi hiyo wakati KMKM ikijiandaa kwenda Kinshasa kwa mechi ya marudiano ya Kombe la CAF dhidi ya DC Motema Pembe.
"Bushiri aliomba kazi mwenyewe na sisi tuliporudi kutoka DRC tukaambiwa tayari ombi lake limejadiliwa na uongozi umeamua kumuajiri", alisema Mohammed.
Hata hivyo alieleza kuwa hilo ni jambo la kawaida ambalo linalenga kuipeleka timu mbele zaidi ya ilipo sasa, na kwamba uongozi unaamini Bushiri anao uwezo wa kuiletea maendeleo hayo.
Alisema bado uongozi haujasaini mkataba rasmi na mwalimu huyo aliyewahi kuwa msaidizi wa Marcio Maximo Taifa Stars, na kocha wa Zanzibar Heroes mara kadhaa pamoja na klabu mbalimbali hapa Zanzibar.
Hata hivyo, alifahamisha kuwa tayari uongozi wa KMKM na Bushiri wamekubaliana mambo yote ya msingi, na mkataba unaotarajiwa kutiwa saini utakuwa wa mwaka mmoja.
Katika kibarua chake kipya cha kuwafundisha mabaharia hao, Bushiri ambaye mara ya mwisho alikuwa akiinoa timu ya Polisi atakuwa akisaidiwa na Ali Vuai Shein
No comments:
Post a Comment