Habari za Punde

HEKAYA ZA BIBI- TAFAKARI

Ashura M. Hamad (Ummu Ahmad)

Kuna njia mbali mbali za kufikisha ujumbe kwa jamii husika haswa haswa za kuleta tafakari fulani ili ueleweke na jamii hiyo. Hupendezwa na njia hii ya kufikisha ujumbe kwa kituo cha televisheni ya Citizen Kenya . “Tafakari ya babu” Kwa hivyo na mimi nimejaribu kuja na Hekaya za Bibi kwa lengo lile la kufikisha ujumbe.

Bibi yangu alipendelea sana kutoa hekaya zake pale anapoona mambo huenda songo mbingo. Wajua utoto una kero na deko lake.

Siku moja miaka ya zamani , bibi alinipa hekaya moja wakati nilipokataa kukuna nazi. Tafakari ilikuwaje?

Palitokea bwana mmoja wa kigunya huko Tanga mji uliopo Tanganyika. Bwana huyu alikuwa na binti yake mpendwa aliyempenda sana. Pia bwana huyu alikuwa na mke lakini si mama wa binti yake mpendwa.

Kama mama ni mlezi alimfundisha binti yake kazi za nyumbani. Alimtuma na alimuomba kumsaidia kazi mbali mbali za nyumbani lakini Bwana arudipo katika mihangaiko yake alichukia sana kumuona binti yake akifanyishwa kazi za jikoni na za nyumbani husikika akisema , “ kwani kanaolegwa ?” Mama huchukia sana na humuamrisha binti kuacha kazi zote atafanya yeye aliyeolegwa.

Binti hupata kichwa na akajiona na kujitazama wote na alikuwa na hekaya za mama wa kambo si mama. Nae huyo hutokomea na starehe zake.

Siku zikenda mwana hajaolegwa, ndo hajaolegwa! kwahiyo lake likawa kula na kulala. Mtoto wa baba si wa mama, binti akakuwa , kazi ikawa kula na kulala kwani mwaya hajaolegwa! Akanawirika mtoto mzuri, mapozi yamemzidi. Hatimaye posa zikaja , bwana mwenye mafedha yake akataka kuoa.

Chereko chereko harusi ikafika na ndoa ikafungwa heddatul-ashara ya siku ya Ijumaa.

Desturi na mila za watu wa pwani pwani , Biharusi akaondoka na kungwi na wasaidizi wake kumsindikiza biharusi kwake Msambweni , Jumba la kifahari hakuna kisichokuwamo, mweru mweru kunawaka. Bibiye alioona kapata nini tena.. Ada ya makungwi siku saba zikafika wakaondoka fungate limemaliza, bibiye akakabidhiwa nyumba yake sasa kanaolegwa, yupo kwake, akapewa mawaidha mawili matatu , mabibi hao wakarudi makwao kibarua chao kikaishia hapo.

Bwana alitoka na aliporudi alikuja na kapu hilo! limejaa, makuku yamo humo, msamaki huo mkubwa wa changu, ndizi za mikono na viungo vya mtuzi, bwana ana mafedhaye! Bibiye akapokea kapu akivikodolea macho tu sijui aanze wapi.

Akalichukua samaki hilo akaenda karoni akachukua kumbi na sabuni akalikosha.na kuliogesha. Akachukua kuku akamtia kwenye sufuria na maji akakata viungo na kuteleka bila ya kumkata. Akachukua ndizi akakata kata nazo kwenye sufuria na maji akateleka. Baadae akaweka chuma cha kukaangia samaki chini akajaza mafuta na kumuingiza samaki bila ya kiungo chochote tena chini, ukapikwa wali hapo bila ya kuchaguliwa mchele likawa bondo , yu maji kaona leo mambo yamemfika, bwana aja ayaona mambo hayo , “ wafanyani mbona mambo haya bibiye, kashangaa macho yamtoka aona vioja vipya . Bwana apeleka kesi kwa mkwewe amtia hasara vyakula tele hauna hataa kilicholika. Baba amjia juu mkewe amwambia wamfanyanini mtoto. Jibu lilimuacha mdomo wazi baba Kwani kanaolegwa!! Aibu.

1 comment:

  1. Good, good, namna hii, siku moja moja tuwekee stori kama hizi kwakweli zinatuchangamsha sana na kutukumbusha mengi.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.