IDARA ya mifugo na Uvuvi, imewafunga uzazi mbwa 80 ikiwa ni hatua ya maendeleo ya operesheni ya kupunguza uzazi kutokana na idadi ya wanyama hao kuonekana kuwa wengi na kuzagaa ovyo.
Zoezi hilo ambalo linaendeshwa na Idara hiyo limewahi kufanyika kwa paka ikiwa ni kwa ajili ya kuwahasi kutokana na kuwa wengi mitaani huku wakiwa hawana matunzo.
Miji ya Unguja na Pemba inakisiwa kuwa na paka wanaofikia zaidi ya 17,000 huku mbwa zaidi ya 5,000 na idadi ya wafugaji wa mifugo tofauti wamefikia 35,000 na wavuvi waliopo ni 26,000.
Hatua hiyo imekuja kutokana na wanyama hao kuonekana kuwa wengi na kusababisha kero mitaani.Aidha kutokana na kukosa chanjo za wanyama zinazotolewa, Idara imeamua kufanya hivyo ili kuepusha athari za matatizo ya kichaa cha wanyama kwa wanadamu.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Kassim Gharib Juma, wakati akieleza Kamati ya Baaza la Wawakilishi inayoshughulikia Mifugo, Utalii, Uwezeshaji na Habari, alisema kuwa tayari mbwa 80 wamefungwa uzazi katika kipindi cha mwaka 2010/2011.
Alisema hatua hiyo ilikuwa na lengo la kupunguza wanyama hao kupata maradhi ya kichaa cha Mbwa ambapo maradhi hayo sasa yamedhibitiwa baada ya kupatiwa chanjo.
Kwa upande wa paka waliofungwa uzazi Katibu huyo, alisema ni 115 ikiwa ni hatua ya kupambana na maradhi ya kichaa ambayo nayo huwakumba wanyama hao.
Mradi wa kichaa cha mbwa ulianza rasmi mwaka 2000 chini ya ufadhili wa World Society for protection of animal (WSPA) kwa Unguja na Pemba na mwaka 2010 kwa msaada wa Melinda na Bill Gate Foundation.
Katibu huyo alisema mbwa waliopatiwa dawa za minyoo ni 2,941 huku Punda walioogeshwa kwa kuwakinga na maradhi yanayotokana na kupe ni 1,780 na 356 walipatiwa matibabu kutokana na maradhi mbali mbali yakiwemo madonda yanayosababishwa na kupigwa sana na wachungaji wao.
Matibabu hayo pia yalifanyika kwa ng’ombe wa gari 353 na mbwa waliotibiwa kwa chanjo ya kichaa cha mbwa ambapo Katibu huyo alisema walifikia 1,996.
Hata hivyo aliifahamisha kamati hiyo kwamba huduma katika kituo cha Karantini la Chinjio la Kisakasaka zimeimarishwa kwa kuwekwa huduma za maji na umeme wa uhakika.
Katibu huyo alisema ingawa kituo hicho kimeweza kufikia hatua hiyo, lakini kwa upande wa Pemba bado hawajaanzisha ila tayari Idara imeshakagua maeneo ambayo yatafanyiwa tathmini ili kuchagua eneo litalokuwa linafaa kwa ajili ya kuanzisha karantini.
No comments:
Post a Comment