Habari za Punde

BARUA YA MALALAMIKO YA WAKAAZI WA MJI MKONGWE

Mkurugenzi Mkuu,


Mamlaka ya Hifadhi na Uendelezaji wa Mji Mkongwe,

SLP 4233

Forodhani

Zanzibar.

YAH: TANGAZO LA MAOMBI YA MAONI JUU YA UJENZI WA HOTELI YA KIFAHARI MAMBO MSIIGE NA UIMARISHAJI WA ENEO KWA AJILI YA BUSTANI YA JAMII BAINA YA TEMBO HOTEL NA STAREHE CLUB SHANGANI, UNGUJA:

Tafadhali husika na kichwa cha habari hapo juu. Kwa barua hii tunastakabadhi rasmi maoni ya wananchi watajwa hapo chini kuhusiana na ujenzi wa hoteli katika jengo lililokuwa la Mambo Msiige sanjari na uendelezaji bustani katika eneo la wazi la Shangani kama tangazo lako linavyopendekeza.

Awali, tungependa kutoa malalamiko yetu juu ya kucheleweshwa kutolewa kwa tangazo hili. Tangazo husika limebandikwa leo tarehe 19/4/2011 na watu wasiokuwa wenyeji na kuonyesha kuwa lilipaswa kuwa limebandikwa kuanzia kutoa maoni ni tarehe 8/4/2011.

Hakika jambo hili linapingana kabisa na dhamira nzima ya uwazi na kukaribisha mawazo ya wananchi kuhusu uamuzi huu mliouchukua. Aidha, muda uliobaki kutoa maoni ni mchache hasa ukizingatia kuwa hakutakuwa na kazi kuanzia Ijumaa ya tarehe 22 Aprili 2011, yaani kesho kutwa, mpaka tarehe 27 Aprili 2011.

Iwapo kisheria maoni yetu ni nguzo na kigezo cha msingi kuhusiana na uendelezwaji wa sehemu hii pamoja na Mji Mkongwe kwa ujumla basi Mamlaka haina budi kufafanua utata huu kwetu kama ni kielelezo cha udhati wa kushirikisha wananchi katika maamuzi muhimu ya kitaifa na kijamii.

Aidha, tukiirejea Sheria inayohusu Uhifadhi na Uendelezaji wa Mji Mkongwe, ambayo inatawala masuala ya Ujenzi na Undelezaji wa Maeneo na Mipango Miji na kuainisha taratibu za kufuatwa katika kuendeleza shughuli za ujenzi katika sehemu za miji na hasa eneo la hifadhi. tungependa kuibua na kuchangia masuala yafuatayo ambayo kwa ujumla wake yanatupa wasiwasi mkubwa juu ya usimamizi na utekelezaji wa taasisi yako majukumu iliyopewa kisheria na wananchi wa Zanzibar.

Masuala makuu tutakayoyachangia kwa hatua hii ya awali ni manne: Wito wa Kutoa maoni; Eneo la Bustaini: Eneo la Ujenzi wa Hoteli; na Uzingatiaji wa sheria na taratibu zilizopo:-

1. WITO WA KUTOA MAONI:

Tunakaribisha wazo la kututaka tutoe maoni kuhusiana na uendelezwaji na ujenzi unaotarajiwa kufanywa lakini tunasikitika kuwa mpaka hii leo mbali na fununu zilizotawala na tangazo lililobandikwa bado wananchi hawana kielelezo chochote iwe cha mchoro au cha maelezo ya kina kuhusiana na nini kinataka kufanyika na kwa nini kinataka kufanywa. Ni vigumu kutoa maoni juu ya taarifa tu pasipo uelewa wa kina ya kusudio lililopo. Hivyo, haja ya Mamlaka kutaka kupokea maoni inakwazwa na kushindwa kwake kutoa maelezo ya kina kwa wananchi kuhusiana na kipi wangependa kitolewe maoni kwa maana ya kuwapa vithibiti au mapendekezo ya mipango mfano mchoro husika kama inavyotakiwa kisheria na kitaratibu.

Kwa hivyo katika eneo hili madai yetu ni :

a) Kutotosha muda wa kutoa maoni kwa vile tangazo lilichelewa kubandikwa na kwa hivyo muda huo uanze upya

b) Kutokuwepo na fursa ya kuona michoro na kwa hivyo michoro hiyo ielekezwe itapatikana wapi ili watoa maoni waweze kuiona na kuitole maoni



2. ENEO LA BUSTANI:

Suala la kuendelezwa kwa eneo la wazi lililopo baina ya Starehe Club na Tembo Hotel kwa matumizi ya jamii ya Shangani na vitongoji vyake na wanachi wa Zanzibar kwa ujumla ni wazo tunalolikaribisha ila tunataka kuthibitishiwa kimaandishi kuwa uendelezaji huo utazingatia na kufuata mapendekezo yaliyomo katika Mpango wa Uhifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe wa Zanzibar (Zanzibar: A plan for the Historic Stone Town) ambayo imeambatanishwa na barua hii.

Katika eneo hili madai yetu ni:

a) Kuweza kuona ramani ya bustani ili kuthibitisha ni eneo kiasi gani litatumika kwa bustani na kiasi gani pengine kwa maegesho ya magariau kumezwa kama sehemu ya ujenzi

b) Kuona michoro ili kuthibitisha kwa kiasi gani bustani hiyo itakuwa ya umma

c) Kuona michoro ili kuwa na uhakika kuwa fursa ya kutumia fukwe (easement) itaendelea kuwepo kwa wananchi



3. ENEO LA KUJENGWA HOTELI:

Tangazo linatuarifu kuwa kuna mpangpo wa kujenga Hoteli ya Kifahari lakini halituelezi wapi kati ya sehemu iliyokuwa Starehe Club na Mambo Msiige na Kiwanja kilichozungumziwa hapo juu itajengwa hoteli hiyo. Ila tumeshuhudia kuwa idara kadhaa za serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambazo zikitoa huduma nyeti kwa jamii ya Zanzibar zikihamishwa ili, inavyobainika sasa, kupisha huo mradi wa ujenzi wa hoteli ya kifahari.

Igawa idara zote zilizokuwemo Mambo Msiige zimehamishwa na hata baadhi ya miundo mbinu kuondolea mpaka sasa hakuna mchoro au kithibiti chochote kilichowekwa kutufahamisha wananchi na wakazi sura ya nini kinatarajiwa kufanyika ingawa eneo lote hilo kwa muda sasa limezingirwa na mabati.

Mambo Msiige ni urithi mkubwa kwa nchi yetu. Pia ilikua ni hazina ya nyaraka muhimu zinazowahusu wanzanzibari katika maisha yao ya kila siku jambo ambalo linahusiana kabisa na uhifadhi ya masuala ya kale na historia kwa ujumla. Kwa kuzingatia ukweli huu, iweje Mamlaka inayosimamia uhifadhi wa Mji Mkongwe iruhusu kuhamishwa kwa nyaraka muhimu kwa manufaa ya wageni na si wakaazi wa Zanzibar? Pia iweje Mamlaka ijihusishe na ukiukwaji wa lengo la kuwepo kwake kwa kuurushu mradi ambao kimantiki unakwenda kiyume na uhifadhi wa shemu nyeti kama ya Mambo Msiige.

Katika eneo hili madai yetu ni kama ifuatavyo:

a) Kuona michoro ili kujua ni kwa kiasi gani mjenzi ameelekeza kutekeleza masharti ya kibali chake cha ujenzi kuhusiana na suala la uhifadhi wa jengo hilo

b) Kuweza kujua ni vipi atalitumia eneo ambalo lilikuwa ni Starehe Club katika kuliunganisha na jengo kuu la Mambo Msiige

c) Kueleweshwa masuala ya SIA na EIA yamefanywa kwa kiasi gani na yatakuwa endelevu kwa kiasi gani

d) Kukutanishwa na wajenzi ili kuweza kueleweshwa na mapema na kuwasiadia fikra katika suala la ajira kwa vijana wa Kizanzibari.



4. UZINGATIAJI WA SHERIA NA TARATIBU ZILIZOPO

Ndugu Mkurugenzi Mkuu, kama tulivyokwisha ainisha hapo juu, na kama taasisi yako inavyokuwa na kawaida ya kutukumbusha wakazi wa Mji Mkongwe kuwa kuna taratibu zinazo ongoza Sheria ya Uhifadhi ya Mamlaka ya Mji Mkongwe, Mipango Miji, Masuala ya matumizi ya ardhi na hata uwekezaji.

Tayari tumeshagusia suala zima la kuwepo kwa michoro kabla ya kuidhinisha kibali cha ujenzi. Pia tumegusia suala la kuomba maoni ya wananchi baada ya kuwa Mamlaka na Wizara ishafanya maamuzi. Kwa nafasi hii tungependa pia kulizungumzia suala la sheria zinazoongoza na kusimamia ukodishwaji wa ardhi na majengo kwani ingawa Sheria ya Ardhi ilifanyiwa marekebisho ili kukidhi mahitaji na kodi za ardhi kauli ya Waziri wa Ardhi na fununu zilizopo zinaashiria kuwa masharti haya mapya hayajazingatiwa kwa muekezaji anayepewa eneo tunalolizungumzia. Hivyo, tungependa kupata uhakika wa suala hili kimaandishi.

Katika eneo hili madai yetu ni:

a) Marekebisho ya sheria yafanyike ili suala la maoni ya wadau au wananchi yawe na maana na sio ilivyo hivi sasa ambapo wakati maoni ya wananchi yanaitishwa basi mjenzi tayari ameshapewa vibali vya ujenzi na kwa hivyo maoni yaioitishwa hayana au hayatakuwa na maana yoyote ile.

Tunarudia tena kupongeza uamuzi wa kukaribisha maoni ya wananchi wa Zanzibar na wakaazi wa eneo la Mji Mkongwe juu ya mradi unokusudiwa kufanyika katika eneo husika na kukiendeleza kiwanja kilichopo baina ya Hoteli ya Tembo na iliyokuwa Starehe Club. Tunachosisitiza na kukifuatilia ni haja ya kufuatwa sheria na kushirikishwa jamii kidhati.

Bila ya shaka Mamlaka husika, Wizara na Mwekezaji mtarajiwa watazingatia maoni na matakwa yetu kama tulivyoainisha awamu hii ya awali. Uhakika tunaoutafuta ni uendelevu wa miradi inayobuniwa pamoja na unendelevu wa Mji Mkongwe kwa namna itakayoleta faida kwa jamii pamoja na vizazi vyetu. Hili basi lifanyike kwa kuzingatia sheria na kanuni zinazoongoza na kusimamia taratibu za majenzi katika Mji wa Zanzibar.

Ahsante.

Kny ya Wananchi.



……………………….. ………………………. ……………………….

Hamid Abubakar, Sk Muhammed Idriss, Abubakar A. Shani

Nakala :-

Rais wa Zanzibar, Dr. Mohammed Ali Shein.

Makamo wa kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif S Hamad.

Makamo wa Pili wa Rais Zanzibar, Balaozi Seif Iddi.

Spika, Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Jaji Mkuu Zanzibar.

Waziri, Maji Majenzi, Nyumba na Makaazi Zanzibar.

Waziri wa Sheria na Utawala Bora Zanzibar.

Mwanasheri Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Kamati ya Baraza la Uwakilishi Masuala ya Jamii

Kamati ya Baraza la Uwakilishi Masuala ya Jamii

Katibu Mkuu Wizara ya Maji Ujenzi Zanzibar.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Zanzibar

Mwakili Mkaazi UNESCO Tanzania.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.