Habari za Punde

HEKAYA ZA BIBI - USTAARABU WA KIUNGUJA!

Ashura M. Hamad (Ummu Ahmad)


Jamani ! Jamani! Karibuni tena katika hekaya za bibi.

Jikumbuke! Ufikirie na utafakari. Bibi aliwahi kunisimulia kisa kuhusu ustaarabu hasa katika chakula.

Ustaarabu unatokana na mila na desturi za mahali, ustaarabu pia unatokana na hulka na tabia ya mtu. Neno ustaarabu linatumika kuwa ni sifa njema lakini pia hutizamwa ustaarabu wenyewe.

Nilikuwa nimechoka baada ya kurudi skuli kijua ndii! kikali cha saa saba mchana. Njaa imenibana. . Unajua mchana unataka kula wali kwa mchuzi na maharagwe au kwa rosti la nyama au mapochopo.

Duh! kwa bahati mbaya siku hiyo mchana kulipikwa muhogo wa nazi . Aaaah! Nilipatikana kwa kuwa muhogo wa nazi siupendi, nilinuna. Bibi akaniambia nimekuekea muhogo wa kuchemsha na papa mkavu wa kuchoma nile kwa chai. Nongwa zikazidi, Bibi na mjukuu wake. Ah! Kwani nilibembelezwa nikaambiwa kama hutaki katafute kijuzuu uende zako chuoni maana muda ulifika. Nikatoka nimenuna. Mashavu mbwii na shingo upande. Njaa ! huwezi kupingana nayo, kidume. Saa tisa niliaga chuoni naumwa kumbe njaa na nilipofika nyumbani nikapapia muhogo wangu kwa papa wa kuchoma na chai. Wee! Vilikuwa vitamu.

Bibi akaanza hekaya zake….

Zamani baada ya Mapinduzi, kulitokea bwana mmoja alikuwa na rafiki yake mrima. Unajua zamani urafiki ulivaana ukawa udugu, watu walipendana na walitembeleana. Sio sasa tunaoneana choyo na husda ushoga huku mwenzio anakung’ong’a.

Bwana huyo alikuwa na safari ya kumtembelea rafiki yake huko Mrima. Alimtumia barua kuwa atafika na mkewe siku kadhaa zijazo.

Safari iliwadia bwana na bibi wakawa safarini, walifika jioni na walilakiwa vizuri na wenyeji wao. Wakakaribishwa na wakapokewa. kila mahali na ustaarabuwe, walijitahidi kutokana na mila na desturi zao.

Safari ndio safari machofu unakuwa nayo. Baada ya kukoga wageni walikaribishwa sebuleni kwa maandalizi ya mlo. Kuliandaliwa sinia hilo limekamilika. Wenyeji wakaa na wageni wao na kuanza kutabaruku huku wakipigishana stori na kukumbushana mambo mbali mbali. Wenyeji wakawasisitiza wageni wao wale washibe wajisikie wapo nyumbani. Bibi wa Unguja akawa na mapozi anakula kwa ncha ya vidole sijui aliona
aibu au ndio ustaarabu wa kwao? Kula bibi aliambiwa. Nakula . alijibu bibiye kwa sauti yambwembwe huku akiona haya.

Baadae akasema kishashiba. Akaletewa maji akanawa. wengine wakaendelea na stori. Bibie akaenda kupumzika machovu yamemzidi na uustaarabuwe. Watu wakala wakamaliza na vilobaki wakapata wengine unajua tena wengine husubiria masanzo wamalizie. Vyombo vikaondoshwa na vikakoshwa na kukasafishwa. Wenyeji wakaamruhusu mgeni wao akapumzike. Na wenyeji nao wakaenda zao kupumzika usiku uliwadia.
Usiku ukayoyoma bwana anakoroma ameshiba ndwii. Bibi anabiruka huku na huko tumbo linampara, Njaa!! Njaa njaa ikawa inalia , tumbo likashindwa kustahamili, bibi yu maji, anahaha afanyeje ? Akatoka chumbani pole pole hadi sebuleni labda kumebakishwa. Peupe na safi kumeshafagiwa hakuna hata chembe ya mkate. Akatoka hadi jikoni para! Para! Anaburuta viatu. Walosikia wakaona anakwenda maliwatoni.

Kufika jikoni akawa paka mwizi anafungua vyungu kuangalia kilichopo.. mwisho akaona mapande ya nazi yaliyovunjika vibaya akabeba mbio mbio akalitumbukiza mdomoni kukata kwa meno . Wee! Si fuu limchome mdomoni, madamu tele yalimwagika vilio, maumivu na njaa juu. Ahh!! Bibiye aliliangusha lio hilo. Watu wote waliamka kukimbilia kulikoni kujua kulikoni? Bwana nae mbio kufika aibu hata kuwatizama wenyeji wake. Mke wake kamtia aibu ugenini. Bibi nae mdomo huo umevimba limekuwa domo tena si mdomo. Ustaarabu wa Unguja mpaka kwenye kula. Jamani Ustaarabu ni kwengine si kwenye kula jamani.

2 comments:

  1. Hahahaaa!!!!!!! kwakweli inapendeza sana, nimeipenda tena sana. inanikumbusha mbali.

    tafadhali usiache kutuaandalia nyengine

    ReplyDelete
  2. inafunza sana pamoja na kufurahisha kwa kweli wadau tuko wengi sana tunaopenda makala kama hizi naungana na mdau wa kwanza hapo juu usiache kutulitea uhondo km huu tunajifunza mengi ndani yake.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.