TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MUSWADA WA KUUNDWA KWA KAMISHENI YA MAREKEBISHO YA KATIBA MUUNGANO
Kesho wananchi wataanza kutoa maoni yao kuhusu Muswada wa kuundwa kwa Kamisheni ya Kukusanya maoni kuhusu kutungwa kwa Katiba mpya ya Jamhuri Muungano wa Tanzania Visiwani Zanzibar.
Mkutano wa kwanza utafanyika katika ukumbi wa Salama Hoteli ya Bwawani kuanzia saa 3:00 asubuhi ambapo wanazuoni, wananchi kwa ujumla watatoa maoni yao mapendekezo ya kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Nchi ya mwaka 2011.
Muswada huo utakaowasilishwa Bungeni wiki ijayo, unakusudia kuweka masharti ya uanzishwaji wa Tume,pamoja na Sekretarieti kwa madhumuni ya kuendesha na kusimamia mchakato wa mabadiliko ya Katiba pamoja na masuala mengine utaangalia chimbuko na mahusiano ya Katiba iliyopo kwa kuzingatia uhuru wa wananchi,mfumo wa siasa, demokrasia na utawala bora.
Ikiwa muswada huo utapitishwa na kuwa Sheria, kutakuwa na utaratibu wa kisheria utakaowezesha Rais kuunda Tume ya kukusanya maoni kuhusu Katiba na kuunda Bunge la Katiba kwa madhumuni ya kutunga Katiba mpya.
Zanzibar ni eneo moja lililoteuliwa kwa wananchi kutoa maoni yao, eneo jengine ni Mkoa wa Dar es Salaam na Dodoma kwa upande wa Tanzania Bara.
Jumapili tarehe 8/04/2011 kutakuwa na mkutano mwengine katika ukumbi wa Skuli ya Haile Selassie saa 3:00 asubuhi.
Mikutano yote hiyo itatangazwa moja kwa moja na vituo vya Radio na Televisheni, hivyo wananchi wanaweza kufuatilia kupitia vituo hivyo.
IMETOLEWA NA:
IDARA YA HABARI(MAELEZO)
ZANZIBAR
07/04/2011
No comments:
Post a Comment