MAOFISA wa Wizara ya Kilimo na Maliasili Pemba wametakiwa kushirikiana na wajasiriamali wadogo wadogo kwa kuwasaidia katika kuongeza uzalishaji bidhaa zenye ubora. Waziri wa Kilimo na Maliasili Mansoor Yussuf Himid, alieleza hayo alipotembelea na kuangalia bidhaa zinazozalishwa na mjasiriamali Omar Ahmed zinazotokana na maziwa ya ng’ombe huko Misufini Chake-Chake Pemba.
Alisema kuwasaidia wajasiriamali hao kuzalisha bidhaaa zenye ubora kupunguza uagiziaji wa bidhaa kutoka nje ambapo alisema nyingi nyengine zimekuwa hazina viwango na ubora kama za hapa Zanzibar endapo zitaimarishwa ipasavyo.
Waziri Mansoor alisema kuwa ipo haja kwa kuimarisha bidhaa za wajasiriamali wadogo wa ndani ya nchi,kwa vile zimekuwa zikionekana na ubora wa hali ya juu. “Watu hawa na wengine kama hawa wanahitaji kupewa msukumo kwa kuwezeshwa wapate kuongeza uzalishaji,kwani bidhaa kutoka nje zimekuwa zikipanda bei siku hadi siku na hata viwango vyake vimekuwa havitambuliki vyema”, alisema Mansoor.
Aliongeza kuwa ipo haja kwa serikali kuwaimarisha wajasiriamali hao kwa kuwawekea mazingira bora ya uzalishaji sambamba na kuwatafutia masoko kwa vile kuwepo kwa masoko ya ndani na nje kutawasaidia kutangaza bidhaa zao na kuitangaza serikali.
Mapema Omar Ahmed alisema wamekuwa wakijitahidi katika kuzalisha bidhaa bora kama vile maziwa,mtindi,samli na siagi lakini wamekuwa wakikumbana na chamngamoto mbali mbali zikiwemo zile za kukosa vifaa vya kufungia bidhaa hizo kitaalamu.
Hivyo aliiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuwasaidia wajasiriamali hao, kuwarahisishia kupata njia bora ya kufunga bidhaa zao zitakazokwenda sambamba na ushindani wa soko la ndani na nje.
No comments:
Post a Comment